Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UKATILI KATIKA FAMILIA: Ndoa zilivyogeuka pango la mauti

87760 Pic+ndoa UKATILI KATIKA FAMILIA: Ndoa zilivyogeuka pango la mauti

Fri, 13 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hellen Igungi anaishi peke yake na watoto wake watatu baada ya kupata kipigo kutoka kwa mumewe, ambacho anaamini kuwa kama si majirani kwa sasa angekuwa maiti,

Alikuwa akipigwa na mumewe huku mageti ya nyumba yao yakiwa yamefungwa, hivyo majirani kushindwa kuingia kumuokoa hadi walipoona hali inakuwa ngumu na hivyo baadhi wakaruka ukuta.

“Nililia kwa nguvu nikisema ‘nakufaa nisaidieni’. Kweli waliingia kunisaidia na hiyo ikawa pona yangu,” anasema Hellen katika ushuhuda wake kuhusu ukatili wa wanaume katika ndoa.

Hellen alinusurika, lakini wako wengine wengi ambao wamepoteza maisha wakiwa ndani ya ndoa kutokana na vipigo ambavyo vingezuilika kama hatua nyingine zingechukuliwa.

Sheria ya Ndoa inakataza upande mmoja wa wanandoa kutoa adhabu kali ya kipigo kwa mwingine, lakini msemaji wa polisi nchini, David Misimbe anasema takwimu za mwaka jana zinaonyesha kuwa wanawake 137 waliuawa kwa kupigwa na waume zao kati ya Januari na Desemba.

Pia, anasema kati ya Januari na Septemba 2019, idadi ya wanawake waliouawa ilikuwa imefikia wanawake 120, likiwemo tukio maarufu la Naomi Marijani (36), mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam, ambaye alipigwa hadi kufariki dunia na baadaye mwili wake kuchomwa moto na mabaki kufukiwa shambani.

Jumla ya vifo vya aina hiyo ndani ya mwaka mmoja na nusu ni 257, hali inayofanya taasisi hiyo ya kwanza katika kuunda jamii na ambayo huanzishwa kwa shangwe, kuanza kuonekana hatari, hasa kwa wanawake.

“Sababu zilizobainika baada ya uchunguzi wetu ni pamoja na wivu wa mapenzi, ulevi na ugomvi mwingine,” anasema Masimbe.

Lakini kwa wanaharakati wa haki za wanawake wanaona sababu hizo ni nyepesi na haziakisi tatizo kubwa lililoko kwenye jamii, ambalo wanaona ni mfumo dume.

Lakini baadhi ya viongozi wa dini wanaona kukosekana kwa mfungamano kwenye ndoa kunaweza kuwa sababu ya ndoa sasa kufikia hatua ya wanandoa kuuana.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani, Mkoa wa Dar es Salaam Sheikh Alhad Mussa anasema hali hiyo inatisha.

“Ndoa ni mafungamano ya mapenzi huruma na kusaidiana, inapotokea hali kama hii inatisha sana,” alisema Sheikh Alhad Mussa.

“Tatizo tunaangalia tulipoangukia, hatuangalii wapi tunakosea. Tunakosea kwenye msingi wake.

“Si kila mwanaume anatakiwa kupewa mke au kila mwanamke anatakiwa kupewa mume.”

Lakini mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga anasema utu umeondoka ndani ya jamii.

Kama ilivyo kwa Jeshi la Polisi, Henga naye anataja suala la ulevi kuwa ni chanzo cha ukatili ndani ya ndoa.

“Tafiti zetu zinaonyesha kwamba ulevi, hasa vijijini unaongeza ukatili na kusababisha vipigo kwa wanawake,” anasema Henga.

Simulizi kwenye ndoa

Lakini Hellen si mkazi wa vijijini, bali Kimara jijini Dar es Salaam, lakini alipigwa na mumewe kwa jinsi ambayo alihisi ingeweza kusababisha kifo chake wakati mumewe alipokuwa akimuadhibu kwa kuchelewa kurudi nyumbani.

“Bahati mbaya sana (siku hiyo) kulikuwa na foleni, hivyo nilichelewa. Nilipofika nilimkuta mume wangu uwanjani, hakujali watoto alianza kunipiga,” anasimulia Hellen.

Anasema ilibidi apige kelele kuomba msaada kwa majirani kwa sababu kipigo kilikuwa kimezidi.

“Nilipiga kelele lakini majirani walipokuja walishindwa kuingia kwa kuwa geti lilikuwa limefungwa,” alisema.

Lakini baadhi ya majirani walilazimika kuruka ukuta ili kumsaidia kwa sababu kelele zake zilizidi.

Mwanamke huyo anasema wakati anasaidiwa alikuwa tayari amejeruhiwa usoni, ikabidi apelekwe polisi na baadaye hospitali kwa ajili ya matibabu.

“Kwa hiyo nikaanza tena kugharamia matibabu. Pesa ambayo tungetumia kwa maendeleo ya familia, nilienda kulipa hospitali,” anasema Hellen.

Pengine katika mambo yanayoweza kuchochea kuendelea kwa ukatili huo ndani ya famili, ndugu zake Hellen wakamshauri asifungue kesi badala yake waende kanisani ili viongozi wa dini wasaidie kutatua mgogoro wake na mumewe.

“Kusema kweli ilikuwa tukiongea na wachungaji anakaa miezi miwili bila kunipiga, nikikosa kidogo tu napigwa mpaka nazimia. Mwisho niliamua kukimbia na watoto na mpaka sasa sijarudi, niliogopa naweza kufa bure,” anasema.

Lakini tukio lililotikisa nchi na kuacha hofu katika ndoa ni la kifo cha Naomi pia wa jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Camillius Wambura alisema mume wa mwanamke huyo, Khamis Luwoga maarufu kama ‘Meshack’ alikiri kumuua mkewe.

Mwanaume huyo anadaiwa kumuua mkewe kisha kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa na kwenda kufukia mabaki shambani kwake.

Tukio jingine ni lile lililotokea Mei 28, 2018 likimhusu Victoria Salvatory (58) anayedaiwa kumuua mumewe, Salvatory Iteganira (62) mkoani Kagera kwa madai ya wivu wa kimapenzi.

Ripoti ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa na Uhalifu (UNODC) ya mwaka 2018, inasema nyumbani ni mahali hatari zaidi kwa wanawake na hususan kwa mauaji na ukatili.

Ripoti hiyo inasema wanawake 87,000 waliuawa duniani mwaka 2017, huku 50,000 au asilimia 58 ikiwa ni mikononi mwa wenzi wao au jamaa watu wa familia.

Idadi hiyo inamaanisha kuwa wanawake 6 waliuawa kila saa moja na watu wanaowafahamu duniani kote.

“Wanawake wanaendelea kulipa gharama kubwa kutokana na kutokuwepo usawa wa kijinsia, ubaguzi na tabia mbaya. Pia wana uwezekano mkubwa wa kuuawa na wapenzi wao na ndugu wa karibu katika familia,” alisema mkurugenzi mtendaji wa UNODC, Yury Fedotov wakati ripoti hiyo ilipotoka Machi, 2018.

Viongozi wa dini wazungumza

Wakati idadi ikionekana kuwa kubwa, viongozi wa kidini wanaona mafundisho ya kuvumiliana pia yanachangia mwenendo huo.

“Unavumiliaje kipigo kinachohatarisha uhai wako?” Anahoji mchungaji wa Kanisa la Elgibo la Tabata, John Paul.

“Nani anasema uvumilie maumivu ambayo mwisho wake ni kuchomwa kwa gunia mbili za mkaa? Hapana, ndoa zinahitaji msaada mkubwa.”

Anasema kinachoweza kuokoa ndoa ni misingi ya maadili inayopaswa kujengwa kwenye familia.

Anaeleza kuwa wanandoa wengi wanaoana bila kupata muda wa kujuana kiundani jambo ambalo ni hatari zaidi.

Naye Mchungaji Samwel Lwiza anasema: “Bado tafsiri ya ndoa inatakiwa iangaliwe tena, kwa sababu wanawake wanavumilia kipigo badala ya kuvumilia maisha yanayohusisha kipato na matumizi, hali ya juu na hali ya chini.”

Sheikh Alhad anasema anayepaswa kupewa mke ni mwanaume mwenye sifa ya huruma, upendo, ubinadamu na utu.

“Sio mwanaume anakuja na pesa zake hatujui historia wala maadili yake, anakuja tu na pesa na kupewa mke,” anasema na kuongeza;

“Imekuwa kawaida mtu anatoka nje huko anakuja amepanga, anaenda kuposa na kupewa mwanamke hajulikani ametokea nchi gani? Hajulikani kama muuaji tunakuja kulalamika tulipoangukia ila hatujihadhari tulipojikwaa.”

Anasema matokeo ya kuozesha wake watu wasio na sifa za kuoa ni vipigo visivyo na huruma na mauaji.

Kwa upande wake, mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Mbezi Beach, Christosiler Kalata alisema msamaha unaweza kusaidia wanandoa kuimarisha mahusiano yao.

“Wanapopigana mbele ya watoto, wanajifunza nini? Watoto nao wakikua watakuwa makatili hivyo hivyo,” alisema Kalata.

Ushauri kumaliza ukatili kwenye ndoa

Henga anashauri kuwepo kwa sheria ya jinsia itakayosaidia kupunguza tatizo hilo.

“Sheria ya jinsia itasaidia sana, watu watashtakiwa moja kwa moja chini ya vifungu vya sheria kulingana na makosa hayo tofauti na wakati huu ambao hata hilo dawati la jinsia bado lipo chini ya sheria nyingine,” alisema Henga.

Anasema tafiti zao zinaonyesha matukio hayo yanaongezeka na kibaya zaidi yanafanyika ndani ya familia.

Columnist: mwananchi.co.tz