Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: naye arudi katika chama chake tu

44868 Uchokozipic UCHOKOZI WA EDO: naye arudi katika chama chake tu

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kila mtu arudi kwao. Hesabu za siasa zama hizi zinawachanganya Watanzania kuliko nyakati nyingine zozote. Wajina wangu, Edward amerudi katika chama chake. Anataka kula pensheni yake bila ya usumbufu. Amenyoosha mikono juu.

Wanasiasa walipiga hesabu zao kwa kutumia utawala wa Mkwere, lakini siasa za sasa sio kama za ‘uncle JK’. Hizi ni ngumu. Wajina wangu amezisoma akazielewa akaona bora aachane na ndoto za urais.

Uamuzi wa Edward mwenzangu ukanifanya niwaze kuwa ni bora hata Braza Zitto Kabwe naye akarudi nyumbani tu kwa akina Freeman. Siku hizi adui yao amekuwa mmoja, wanaongea lugha moja, wanatabasamu pamoja. Arudi tu mpaka labda upepo utakapobadilika miaka kadhaa ijayo anaweza kutibuana nao tena.

Katika chama chake Namba Moja amemvuruga. Kamchukua ‘mama’ kampa mkoa kule Kaskazini. Kamchukua ‘Profesa’ kampa ukatibu mkuu. Sasa aliye kifua mbele amebaki peke yake. Siasa anazigonga vizuri kwa kutumia kauli na njia zile zile za rafiki zake wa zamani.

Wamekuwa marafiki tena. Upepo mkali wa siasa umewarudisha pamoja. Anawatetea maadui zake hadharani na wao wanamtetea, wanatumia hoja zake kuthibitisha hili na lile. Hata yeye anatumia hoja zile zile. Wamekuwa marafiki wakubwa.

Hatukutegemea haya kwa haraka namna hii, lakini yametokea. Kitu cha kujifunza ni wanasiasa kuangalia zaidi mbele. Zitto alikuwa anashutumiwa na wenzake kwamba alikuwa kipenzi cha chama tawala. Kama ni kweli basi hakujua kwamba ndani ya chama tawala yangeweza kutokea mabadiliko ambayo yangemgusa na yeye kiasi cha kutokea mtu ambaye angekivuruga chama chake kabisa.

Kama chama chake kilikuwa tatizo dhidi yake, basi nacho hakikujua kwamba siku moja kingemuhitaji Zitto katika mapambano. Nadhani Namba Moja amewafundisha kuziangalia siasa kwa mbali zaidi. Utawala uliopita uliwafundisha kuziangalia siasa kwa karibu.

Kwa sasa wanazungumza lugha moja katika kila kitu. Nadhani wataishi katika maisha ya Ukawa. Tatizo wananchi watakuwa wanawahoji. ‘Sasa nyie tatizo lenu lilikuwa nini?’. Mwingine atauliza ‘mbona mnatuletea mezani vyama tofauti wakati kila kitu mnazungumza lugha moja na mnakunywa chai pamoja?’.



Columnist: mwananchi.co.tz