Edward Lowassa amerudi CCM, Maalim Seif amekwenda ACT. Ghafla msajili anaipa ACT siku 14 ijieleze kwa nini isifutwe kwa makosa mawili makubwa. Mara siku 14 zinafika. Utetezi haujitoshelezi, kinafutwa.
Maalim Seif na Zitto Kabwe wanapigwa na mshangao. Wanajiuliza wafanye nini?. Wanafungua kesi mahakamani. Muda unayoyoma. Wanaona haitoshi. Wanafanya kile ambacho Seif alikifanya akiwa CUF. Wanahamia Chadema.
Huyu Zitto inakuwa kama amerudi nyumbani. Kwa Maalim inakuwa mara ya kwanza kuwa Chadema. Mshale wa saa unayoyoma. Ghafla Machi imefika, Chadema wanaandikiwa barua ya kujieleza kwa nini chama chao kisifutwe. Akina Halima Mdee wana uwezo wa kufanya vurugu muda wowote wale. Siwaamini.
Ghafla wanatiwa hatiani na usajili wao unafutwa. Mshale wa kuelekea katika saa ya uchaguzi unayoyoma. Wananchi wanapigwa na butwaa, lakini vyama vya siasa bado vingi. Uchaguzi unakaribia. Professa Lipumba anatangaza kugombea Urais. Mzee John Cheyo naye anamtangaza mwanachama wake fulani kugombea urais.
Unashangaa nini? Ni uchaguzi halali wa vyama vingi. Mpambano unaanza taratibu kwa kampeni za hapa na pale. Bado unaendelea kusoma kolamu hii? Nilikuwa natania tu. Sipo ‘serious’ sana. Nilikuwa najaribu kutabiri tu. Ni utabiri wa hali ya hewa tu.
Nilijikuta ghafla nikiwaza haya baada ya msajili kumuandikia barua Zitto na wenzake. Kitatokea nini kama ACT itafutwa? Maalim na Zitto watakwenda wapi? Wataanzisha Chama chao au watakwenda Chadema? Halafu nini kitafuata?
Siasa zetu zimeanza kwenda kasi kuelekea uchaguzi wa mwaka 2020. Jinsi ambavyo wajina wangu Edward amerudi chamani. Jinsi ambavyo Maalim amekwenda ACT. Jinsi ambavyo msajili ametishia kukifuta chama chao.
Hivi lile kosa la kushindwa kuwasilisha hesabu za ukaguzi sijui kwa nini halikuwasilishwa kabla ya Maalim kuhamia ACT? Halafu hili la kuchoma moto bendera linafikirisha kidogo. Walianza kuchoma wakahama, au walihama wakachoma? Walifanya kosa wakiwa wanachama wa chama gani?
Vyovyote ilivyo pole nyingi zimuendee Zitto popote alipo. Anapambana kweli kweli katika twitter na Instagram, lakini wenzake wanajua namna ya kumbana kwingineko. Vigogo wake walichomolewa mmoja mmoja wakawa mabosi serikalini. Akafanya usajili wa kutisha wa kumnunua ‘Lionel Messi’ kutoka Zanzibar lakini kumbe sasa timu yake inaweza kufutwa. Siasa bwana!