Tuanzie wapi jamani? Dodoma au Mtwara? Muda ni mchache mambo ni mengi. Maisha yanakwenda kasi. Nchi inakwenda kasi. Tuanzie kwetu Mtwara. Namba Moja yupo huko akiendelea na ziara yake. Hatuwezi kuanza na Dodoma wakati Namba Moja anafanya kazi zake.
Alikuwa Mtwara kutuliza fukuto. Nilitabasamu nilipowaza kama alikuwa anakwenda ‘kuwachapa bakora wao na shangazi zao’ lakini mwishowe aliwaambia “anawapenda sana”. Hotuba yake ilikuwa maridadi. Nadhani wasaidizi wake walimwambia ukweli na akajaribu kwenda na ukweli huo.
Nilikuwa Mtwara, Februari mwaka huu. Namba Moja amejibu maswali ambayo hayakuwa na majibu wakati nilipokwenda Mtwara. Upepo ungevuma kama nilivyouacha nadhani kipute cha 2020 kingemsumbua kule Kusini.
Suala la Kangomba nitarudi hapa kulielezea wiki ijayo.
Namba Moja amewasamehe hawa jamaa na watalipwa noti zao kama kawaida. Hapo pia amezichanga karata zake vyema. Kuna vitu ni vigumu kuviondoa njiani ghaflaghafla.
Twende Dodoma. Ustaadhi Assad alikuwa kikaangoni pale mji mkuu. Waheshimiwa wamesema hawatashirikiana naye. Sisi tulioishia darasa la saba tumechanganyikiwa. Tunajuta kwa nini hatukwenda shule.
Tuna maswali ambayo hayana majibu. Kwa mfano, zamani tulidhani ofisi ya ustaadhi na Bunge wangekuwa marafiki sana na kisha adui yao angeweza kuwa Serikali. Picha tunayopata sasa ni tofauti kabisa.
Inawezekana ni kwa mara ya kwanza tunaona ofisi ya ustaadhi na Bunge vinachuana. Tulizoea kuona Serikali na Bunge vikipambana, au Serikali na ofisi ya ustaadhi vikipambana. Hili la ofisi ya ustaadhi na Bunge kugombana ni jipya kwa sisi ambao tumeishia darasa la saba.
Neno “dhaifu” nalo limeshika chati pale Dodoma. Awamu iliyopita neno hili aliambiwa Namba Moja wa wakati huo.
Safari hii limeambiwa Bunge. Sikumbuki Namba Moja alichukua hatua gani nyakati zile, lakini kitu cha msingi unapoambiwa dhaifu inabidi ujitafakari zaidi.
Ugonjwa mkubwa ambao umeikumba nchi kwa sasa ni kutojitafakari. Ni kweli unaweza kutoa kucha zako, ukafoka, ukatumia makali yako, lakini mwishowe inabidi ujitafakari. “Hivi kweli mimi ni dhaifu?” “Hivi kweli sisi ni dhaifu?” “Zamani wenzetu walikuwa wanafanya kazi kwa mipaka na misingi gani?”