Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO:Wanachonong’onezana kijiweni kuhusu ajali za watumishi wa umma

43824 Uchokozipic UCHOKOZI WA EDO:Wanachonong’onezana kijiweni kuhusu ajali za watumishi wa umma

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bado naendelea kuleta stori za kijiweni kwetu Mwananyamala katika nyanja mbalimbali. Juzi tulizungumza kuhusu vifo vitokanavyo na ajali za watumishi. Kila mmoja akatoa lake la moyoni. Inasikitisha sana. Watumishi wa Serikali kufariki ndani ya saa 72 kwa ajali mbalimbali.

Mzee mmoja akadai kwamba madereva wazoefu wameondolewa kazini kwa sababu mbalimba ikiwamo ya kutoa nafasi kwa wenye elimu ambapo baadhi ya waliochukuliwa ni wale wa miaka ya karibuni. Hawana uzoefu. Kuna madereva wengi kutoka VETA sasa wamepata kazi.

Akadai madereva wapya hawana ujuzi na barabara na kwamba wale wazoefu walioondolewa kwa kutokuwa na vyeti vya udereva au kushindwa kufika elimu ya kidato cha nne ndio ambao walikuwa wanazijua hizi barabara zetu na mahitaji yake. Wameishi kwa vitendo zaidi kuliko nadharia.

Kijana mmoja anayeongoza kwa ubishi zaidi maskani alitoa hoja kwamba magari ya Serikali yamekuwa yakienda kasi bila ya trafiki kuchukua hatua zozote. Trafiki wakiona magari yenye namba STK, STL, SU huwa wanazima kamera zao na kupisha wakubwa au watumishi wapite.

Aliishindilia hoja yake kwa kudai kwamba Magari binafsi ndio ambayo yanapigwa kamera kila kukicha. Akasisitiza kwamba kinachoonekana ni kwamba watu binafsi hawana sababu ya kuwa na haraka katika safari zao, lakini maofisa wa Serikali ndio wanaoruhusiwa kuwa na haraka.

Akadakia kijana mwingine ambaye huwa anakuja na Biblia yake kijiweni. Biblia haichomoki mkononi mwake. Mara nyingi anatupa mahubiri ya hapa na pale. Labda kwa sababu yeye hajui kucheza bao. Huyu akatuambia kwamba watu wote wanaokufa ‘siku zao zimefika’. Kwamba siku za mwanadamu aliyezaliwa kutoka katika tumbo la mwanamke ni chache.

Hizi kauli za vitabu vya dini zinapaswa kuheshimiwa, lakini kwa mtazamo wangu nadhani tushughulike kwanza na hao watoa hoja wawili wa kwanza kabla hatujakubali hoja ya mwisho ya mhubiri, kwani ajali za watumishi wa Serikali zimekuwa nyingi na hatupaswi kufanya mzaha.

Nimeandika kwa huzuni kubwa. Nataka kuchokoza wenye mamlaka zao wachunguze kwa kina kisha tukishajiridhisha kwamba chanzo cha ajali hizi sio sisi wanadamu wenyewe basi tumuachie Mungu kama alivyosema mhubiri wetu wa maskani.



Columnist: mwananchi.co.tz