Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Waliitwa ‘wazee wetu’ sasa ni wapumbavu

68308 Edo+kumwembe

Fri, 26 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nikamsikia Mzee Ruksa juzi akimruka mheshimiwa wa zamani, Bwana January kuhusu ile picha aliyoweka wakati akikubali kutimuliwa. January aliweka picha yake na Mzee Ruksa. Nadhani hakusoma alama za nyakati. Mzee Ruksa alishazisoma.

Mzee Ruksa akasema “maji yamekwishakorogeka”. Nikacheka sana. Ndio, hali ya hewa sio ile ya miaka yetu. Wengine tumekubali matokeo, wachache hawajakubali matokeo. Ukweli ni kama ule aliousema Mzee Ruksa. Maji yamekorogeka.

Juzi nikamsikia mheshimiwa Katibu akiunguruma. Akawaita wazee wapumbavu na ule waraka wao wa kipumbavu. Haikuwa ajali. Anawakilisha watu kadhaa ambao wanatengeneza chama kipya ndani ya chama cha zamani. Chama kinasafishwa!

Katika mchakato wa kusafisha chama tubakize akiba ya maneno. Tuhifadhi wazee wetu. Tusiwapachike wazee jina la ‘wapumbavu’. Tuendelee tu kuwaita ‘wazee wetu’. Hatupotezi kitu kuwaita hivyo hawa makomredi.

Tunaweza kutofautiana kuhusu misimamo na itikadi, lakini uzee wao unabakia pale pale. Hapo zamani wakati upinzani ukiwa moto waliwahi kuongoza safu ya timu ya nyumbani kupata ushindi murua mara kwa mara. Kuna ‘kaheshima kanahitajika’ kwao.

Zamani wazee wengi walikuwa wanakosea. Bado walihifadhiwa kidogo. Waliitwa ‘wazee wetu’. Hakukuwa na namna ya kuwaita ‘wapumbavu’. wasingeitwa hivyo na wazee wenzao au vijana, lakini sasa vijana wamepewa ‘vifua na misuli’.

Pia Soma

Nilipopita maskani jana rafiki zangu wengine ambao wote tumeishia darasa la saba wakaniambia niwaase vijana wapunguze maneno makali. Mwenyezi Mungu akitupa muda mwingi wa kuishi bado maisha yetu yataendelea kutegemeana.

Vijana wapunguze kutanua vifua kidogo. Twende taratibu. Kuna watu wako kule upinzani wamewahi kubinyana sana na hawa wazee lakini walilihifadhi neno ‘wapumbavu’. kuna maisha baada ya siasa. Kuna maisha baada ya uchaguzi. Kuna maisha baada ya kila kitu.

Kinacholeta tabasamu usoni ni kwamba mtu anayesema fulani ni mpumbavu hajui jamii yetu inamtazama vipi. Hasa pale unapojaribu kukumbuka maisha aliyopitia miezi kadhaa kabla ya cheo chake cha leo, kisha ukalinganisha na maisha yake ya sasa. Si ajabu mioyo yetu inamuona hivyo hivyo lakini bado tunahifadhi neno ‘mpumbavu’.Leo nimekuwa mpole. Nimeandika kwa upole. Lile neno limenishtua kidogo.

Columnist: mwananchi.co.tz