Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Wacheza bao walivyonibana kuhusu Profesa Assad

43590 Edo+kumwembe UCHOKOZI WA EDO: Wacheza bao walivyonibana kuhusu Profesa Assad

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wasomi wa nchi yetu wanatuchanganya kweli tulioshia darasa la saba. Hawajui tu. Kuna wakati tunakuwa bize vijiweni kushabikia mechi za siasa ambazo ghafla hatujui kama zimeisha au mwamuzi bado anachezesha.

Mimi ndio kiongozi wa kijiwe chetu cha wasiosoma huku mtaani kwetu Mwanyamala. Maswali yote yananiangukia kwa sababu nina uwezo wa kusoma magazeti kwa ufasaha kidogo. Juzi wakati tunacheza bao maskani wakaniuliza ‘hivi ile habari ya Professa Assad imeishia wapi?’.

Ghafla nikagundua kwamba swali lilikuwa la msingi. Hivi kweli, habari ya Bwana Msomi Assad imeishia wapi? Aliitwa Dodoma na mkuu wa jengo, zikapigwa kelele nyingi kutoka pande mbalimbali, akaenda na suti na makabrasha yake, akahojiwa, halafu basi.

Wale mambumbumbu wenzangu wasio na shule wakaniuliza, ‘huwa inaishia hivi au inaendelea?’. Sikuwa na jibu lakini nikadanganya kwamba itaendelea tu. Wakaniuliza swali jingine la ghafla. Sikutegemea. “Mbona Zitto naye aliwahi kuitwa na kamati ya maadili akahojiwa na hakuna kilichoendelea mpaka leo?” nikaishiwa pumzi.

Nikaanza kutafakari huku nikicheza bao. Kumbe wananchi huwa wanataka majibu baada ya kesi za haraka haraka nje ya mahakama kama hizi. Hivi baada ya pale kama majibu ya Professa hayakuiridhisha kamati huwa kinafuata nini? Anapelekwa mahakamani au anafukuzwa kazi?.

Endapo majibu yake yaliwaridhisha waliohoji huwa inakuaje? Anasamehewa na kusafishwa hadharani?, na hatima ya aliyemshutumu inakwenda vipi?, niliendelea kucheza bao huku nikitafakari bila ya kuwashirikisha. Mimi ni darasa la saba kama wao, lakini wananiamini sana. Ninapokuwa sina majibu nakuwa bize na bao. Hata Mwalimu Nyerere naye alicheza bao katika baadhi ya mazingira.

Wakati namalizia kucheza mchezo wa mwisho huku nikiwa sina majibu nikagundua njia ya kuwanyamazisha ni kuanzisha mada nyingine. Mimi sio wa kwanza kutumia mbinu hii. Hata hao wanoanzisha kesi wasizoziweza huwa wana tabia ya kupandisha kesi juu ya kesi nyingine.

Kwa jinsi Watanzania tunavyopenda kudakia mada mpya na kusahau ya zamani kwa haraka hapana shaka nilichukua uamuzi sahihi. Unaweza kuanzisha mada nyepesi tu ya jinsi Diamond Platinumz alivyovaa majuzi, watu wakasahau mada nzito ya kisiasa.



Columnist: mwananchi.co.tz