Wabunge wetu bwana! Wako fasta kwelikweli. Kama wanapoambiwa wapitishe miswada ambayo bado haijaeleweka halafu msimamo wa chama ukawa ni kupitisha. Wanapitisha fasta. Nawakubali sana.
Majuzi walikuwa Cairo, Misri. Timu yetu ya taifa ipo kule ikicheza katika michuano ya mataifa ya Afrika. wabunge wakaona hakuna namna ya kupata ‘kiki’ ya haraka haraka zaidi ya kwenda Cairo kuwasapoti vijana. Miaka minne sasa tangu utawala wa Namba Moja ulipoingia madarakani, kuna wabunge hawajavuka hata Namanga au Tunduma. Hii ilikuwa fursa.
Tukafungwa mabao 2-0 na Senegal. Mechi ilipomalizika walirudi na kufanya mkutano na waandishi wa habari pale Airport. Walishutumu mengi na hasa kumshutumu kocha, Emmanuel Amunike. Kwa siku za karibuni ni rahisi kusikilizwa kama ukimlaumu kocha wa Taifa Stars kwa kila kitu.
Hata hivyo, sio wote wana ‘moral authority’ (uhalali) wa kumlaumu kocha. Baadhi ya hawa wanaolaumu ndio wanaopitisha bejeti ndogo zaidi ya michezo pale Dodoma. Ni hao hao ambao wameruhusu tuwe na viwanja vibovu zaidi katika ligi kuu yetu. Viwanja vingi ni vya chama chao.
Kilomita moja kutoka ulipo mjengo wa Dodoma kuna uwanja wa Jamhuri. Katazame sehemu ya kuchezea ilivyo mbovu. Yote haya tunayasahau wakati tunapohoji kichapo cha Cairo. Inachekesha sana lakini hakuna jinsi.
Kichapo cha Cairo kimebebwa na historia kubwa nyuma yake. Yale ni mavuno tu yanayotokana na misingi mibovu tuliyoijenga na tunayoendelea kuijenga kila siku sio katika soka tu bali hata michezo mingine. Vigogo hawakujali sana hayo lakini walikwenda Cairo ili warudi na ushindi. Endapo Stars ingeshinda si ajabu wangesema kwamba wao ndio walisababisha timu ishinde.
Pia Soma
- Wananchi walivyozungumzia kauli ya Jaguar
- Asimulia miaka 18 ya ndoa yake na anayedaiwa kumchemsha mwanae
- Wahamiaji haramu 12 kutoka Ethiopia wakamatwa Morogoro
Hata hii Taifa Stars yenyewe kwa kiasi kikubwa mzigo umebebeshwa pale TFF. Tuna tabia ya kuwapokea wanamichezo waliofanya vizuri nje ya nchi na wakati mwingine tunawapeleka bungeni. Ukichunguza, hawakupatiwa msaada mkubwa huko nyuma.