Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO:Usimwamini yeyote kati ya ATCL na Diamond Platinumz

32352 UCHOKZOZIPIC Diamond Platnumz

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kuna mkanda wa video unaozunguuka mitandaoni ukimwonyesha mtumishi wa ATCL akiweka ngumu kwa mwanamuziki, Diamond Platinumz na watu wake wasipande ndege ya shirika hilo jijini Mwanza kwa madai ya kuchelewa kuwasili uwanjani kwa muda waliotakiwa.

Mkanda juu ya mkanda. Diamond akasema hawakuchelewa bali jamaa waliuza nafasi zao. Kichekesho kingine ambacho kimeanza kuzoeleka kikaja. Bosi mmoja wa ATCL akadai kwamba ‘kwa uchunguzi’ wa haraka waligundua kwamba Diamond alichelewa ndege.

Diamond naye akajibu tena kwa kusisitiza kwamba hakuchelewa ndege. Nadhani stori imekufa hapo. Sidhani kama itaendelea. Kwa waliotaka mwendelezo wasubiri nimalizie hapa.

Usiwaamini wote hao. Labda ni kweli Diamond alichelewa ndege. Si unajua kuna ujana na ustaa ndani yake. Lakini najiuliza, sijawahi kuona Diamond akiingia katika sakata kama hili. Kila siku yuko hewani. Leo Washangton, kesho Ottawa, keshokutwa Mtwara. Labda kwa mara ya kwanza aliingiwa na utoto.

Lakini usiwaamini ATCL pia. Kuna kasheshe kubwa tunazipata katika viwanja vya ndege. Wao na wale mapacha wao waliofungiwa wote ni shida. Lakini zaidi nimekerwa na kile kitendo cha bosi kudai ‘uchunguzi wao wa haraka’ unaonyesha Diamond alichelewa.

Siku hizi umekuwa ni mtindo kwa mtuhumiwa kuendesha mwenyewe mashtaka, kuwa hakimu na kisha kutoa hukumu. Hivi walimwita Diamond kwa mahojiano zaidi awape vielelezo kwa nini anasema hakuchelewa? Hapana. Walichofanya ni kuwapigia simu wale wale watumishi waliorekodiwa, wakadai kwamba Diamond alichelewa, bosi akaitisha mkutano na waandishi wa habari akahukumu kwamba Diamond alichelewa.

Wale maafande waliompiga mwandishi wa habari na picha zikasambaa mitandaoni nao waliendesha kesi wenyewe, wakahukumu wenyewe kwamba mwandishi alitaka kuwapiga polisi. Mwandishi mwenyewe ana mbavu nne tu juu ya tumbo lake. Kesi ikaishia hapo. Hapa ndipo ninapoweka akiba ya maneno. Simwamini yeyote si Diamond wala ATCL. Huku kwa Diamond kama nilivyosema kuna ujana ndani yake. Inawezekana. Upande mwingine nako historia inajirudia kwa mtuhumiwa kuendesha mashtaka na kutoa hukumu. Huwa najiuliza hali hii itaendelea hivi mpaka lini? Hata mbinguni ndio maana kuna Mungu. Kama tungeambiwa tuendeshe kesi zetu wenyewe sote tungesema hatuna hatia. Tungesema huku duniani tulikuwa watakatifu. Nitarudi tena siku nyingine.



Columnist: mwananchi.co.tz