Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Tunakunywa kahawa bifu la Spika na RC

64628 Edo+Kumwembe

Thu, 27 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kahawa kando, kashata pembeni. Wale wenye uwezo wameagiza popcorn. Kwa Kiswahili fasaha cha Mzee Ndimara Tegambwage nadhani popcorn ni bisi. Tupo pamoja tunaendelea kutazama pambano la mkuu wa mjengoni pale Dodoma dhidi ya bosi wetu wa mkoa hapa Dar es Salaam.

Ni pambano kali lakini hatuna cha kufanya. Tunatazama huku tunacheka. Sijui walikorofishana wapi aisee. Tunachojua ni kwamba ilianzia pale Bosi wetu wa mkoa alipoitwa nyakati fulani hivi kwenda Dodoma kuhojiwa kwa kudharau Bunge.

Baadae tukadhani yameisha kumbe bado, likaja lile timbwili la mtu anayeitwa Pierre. Bosi wetu wa mkoa alikuwa na maoni tofauti kuhusu umaarufu ‘wa kipuuzi’ wa Pierre. Aliweka hisia zake wazi na akawagawanya watu. Saa 24 baadaye, Pierre alikuwa ameitwa bungeni na bosi wa mjengoni kwa ajili ya kwenda kusalimia bunge.

Sasa limekuja suala la juzi la mkuu wa mjengoni kudai kwamba wachezaji wa Taifa Stars walifungwa na Senegal kwa sababu hawana lishe. Bosi wetu wa mkoa amekuja juu na kudai mkuu wa mjengo kadhalilisha wawakilishi wa taifa waliopo vitani.

Sitaki kusema nani yupo sahihi. Natazama filamu tu huku nikicheka. Wote hawa tunajua kwamba wapo karibu na Namba Moja. Yule wa kule Dodoma kuna wakati tulihoji ukaribu wake na Namba Moja uliopitiliza kiasi kwamba tukahisi anashusha heshima ya mhimili wake.

Huyu bosi wetu naye tunajua kwamba yuko karibu na Namba Moja. Sasa hatuelewi Namba Moja hapa atamsikiliza nani zaidi, na unapofikia hatua hii kwamba hauelewi Namba Moja anampenda nani zaidi basi inabidi unywe kahawa na kushudia ‘movie’ (sinema) bila ya kupiga kelele. Huku uswahilini tayari watu washaanza kunong’ona “shauri zao bwana watajuana wenyewe”.

Pia Soma

Nahisi kuanza kuingia katika mkumbo huo huo tu wa kusema “shauri zao aisee, watajuana wenyewe”. Tunachosubiri ni kuona awamu nyingine ya bifu lao itawapeleka wapi. Kila mtu anatunisha msuli kwa nafasi yake. Hatuna tatizo na bei ya kahawa, bei ya bando la simu, na bei ya kununua gazeti la Mwananchi. Tupo tayari kuendelea kufuatilia ‘bifu’ lao.

Columnist: mwananchi.co.tz