Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Tumeingia mwaka 2019, macho yote kwa Anko

34461 Edo+kumwembe Tanzania Web Photo

Wed, 2 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati mwingine naishia kucheka jinsi Namba Moja alivyo jeshi la mtu mmoja. Ameweza kuamua anachotaka bila ya shinikizo. Wengine tumeishia kutabiri tu anachoweza kufanya siku za usoni. Kama kuna mwaka tumehisi mengi yanakuja basi ni 2019.

Kuamkia jana tumeingia 2019. Macho yote yanakwenda kwa Mheshimiwa Namba Moja pale Magogoni. Mtaani kuna minong’ono ya aina mbili. Kuna wale wanaoamini kwamba mheshimiwa atalegeza kamba.

Kwamba mwaka 2019 mheshimiwa pia atakuwa anatupia jicho lake katika masuala ya uchaguzi. Wale waliokuwa wanasema ‘vyuma vimekaza’ wanaweza kusema ‘vyuma vimeachia’ na kwenda kupiga kura mwakani wakiamini Namba Moja anafaa.

Watanzania wengi wana matarajio kwamba mwaka mmoja kabla ya uchaguzi lazima fedha iingie katika mzunguko na yale maisha rahisi rahisi ya mheshimiwa aliyepita yatarudi. Wanaosema hivi nawatazama machoni naona hawana hakika sana na wanachokisema.

Eti wanadai kwamba Namba Moja atalegeza kidogo, halafu uchaguzi ukipita akishinda atatuaga kwa kukaza sana. Haya ni mawazo tu.

Wote wanaosema hivi wanaishi kwa mazoea kutokana na awamu zilizopita lakini kuna mazoea mengi ambayo Namba Moja alishatukumbusha kuyaondoa, sasa hatujui kama na tabia hii inabidi tuisahau katika utawala wake au vinginevyo.

Halafu kuna watu wangu wanaomjua vyema Namba Moja. Wanakwambia haigizi na wala hana masihara kwa anachoamini, alivyo ndivyo alivyo. Anachoamini ndicho anachoamini. Siku moja aliwahi kutuambia kuwa hajaribiwi.

Kuna kauli mbili tatu za waziri wetu wa mambo ya noti ambazo zinatia moyo kwamba labda tunakoenda mambo yatalegea. Kauli kama hii ya kuaga mwaka kwamba tusifunge biashara za watu ambao hawajalipa kodi. Labda wakubwa wameanza kuwa na mtazamo tofauti na namna ya kukuza uchumi.

Lakini yote tisa, huu ni mwaka ambao tutapata picha zaidi ya namna ambavyo Namba Moja anavyoufikiria uchaguzi wa mwakani. Tukifika Desemba 31 mwaka huu tutatazama nyuma na kujua kama Namba Moja anatabirika au hatabiriki.

Kwa ninavyompenda Namba Moja ni kwamba hazitapita hotuba zake tano kabla hatujajua kwamba mwendo utakuwa ule ule au atalegeza. Nadhani minong’ono kuhusu mwaka 2019 tulivyousubiri kwa hamu itakuwa imemfikia. Atatupa majibu muda si mrefu. Tusubiri tu.



Columnist: mwananchi.co.tz