Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Tumefika 2019 ghafla bomoabomoa imeondoka

36705 Edopic UCHOKOZI WA EDO: Tumefika 2019 ghafla bomoabomoa imeondoka

Wed, 16 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nataka kuamini kuwa mwanadamu wa Tanzania huwa ana bahati mbaya mara uchaguzi mkuu wowote unapopita na hujikuta ameangukiwa na bahati nzuri mara tu uchaguzi mkuu mwingine unapokaribia.

Wala siamini kama Serikali huwa inafanya makusudi. Nadhani ni ‘bahati mbaya’ huwa inazidiwa na ‘bahati nzuri’ kutokana na nyakati zilizopo. Siamini kama wakubwa huwa wanafanya makusudi. Siamini kabisa. Narudia, siamini kabisa.

Novemba 2015 kulikuwa na bomoabomoa nchi nzima. Picha ya kusikitisha zaidi ni ile ya mama mmoja pale Kinondoni akiwa anamvalisha mwanae nguo za shule wakiwa juu ya matofali ya ‘marehemu nyumba yao’.

Juzi bosi mkuu wa mambo ya ardhi ametangaza kwamba kwa sasa hakutakuwa na bomoabomoa. Tumefika mwaka 2019. Tunaelekea katika uchaguzi mkuu. Nawaza tu kwamba huenda ni bahati mbaya tunapotoka katika uchaguzi mkuu kunakuwa na bomoabomoa, tunapoelekea uchaguzi wakubwa wanaondoa bomoabomoa.

Katika kiingereza kama kile cha gazeti la The Citizen huwa tunasema ni ‘Coincidence’ tu kwamba bahati nzuri nyingi zinaangukia wakati wa kuelekea uchaguzi. Upendo mwingi unaanza kurudi kwa raia. Kinachoshangaza ni kwamba sababu zote mbili za kubomoa au kutobomoa ni imara.

Kwa mfano, hii sababu ya kurasimisha makazi holela ingetolewa Novemba 2015 ingekuwa sababu ya msingi. Kuna watu hawapo maeneo hatarishi na wamevunjiwa nyumba zao. Leo tutawaambia nini?

Pia, zile sababu za baadhi ya wananchi kubomolewa wakati ule zilidaiwa kuwa za msingi kutoka kwa wakubwa wetu. Walisema wengine wamejenga katika vyanzo vya maji na sababu nyinginezo. Zilitolewa sababu nyingi zilizoonekana kuwa nzito wakati ule. Leo vipi tena kuhusu vile vyanzo vya maji?

Tutasikia mengi kuelekea mwakani. Tutapata bahati nyingi. Kuna wale watu jeuri pale Dodoma watasambaa katika maeneo yao na wataanza kupiga magoti. Watapiga magoti hata kwa watoto wadogo. Kisa? Kuomba uhalali wa kurudi tena mjengoni. Hizi ndizo bahati nzuri ambazo tunazipata miezi 24 kabla ya uchaguzi.

Utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kwamba wakati wa wanyonge kutembea kifua mbele umekaribia kwa kasi. Watatembea sana kifua mbele mpaka Novemba 2020.



Columnist: mwananchi.co.tz