Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Tumeacha kusikiliza sauti, tumeenda kuoga

69238 Edo+Kumwembe

Thu, 1 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bosi wa Mkoa wangu wakati mwingine kazi yake ni kulainisha mambo magumu. Akiona watu wengi wameelekea upande wa kushoto yeye anatoa kauli ambayo itawageuza kwenda upande wa kulia. Anaifanya kazi hiyo kwa umaridadi.

Hata kama kushoto ni kutamu, lakini atatupeleka kulia na kutusahaulisha kitu ambacho kilikuwa kinatupeleka kushoto. Wataalamu wa maneno ya mjini kina Inspekta Haroun huwa wanasema,‘ametuondoa njiani.’

Kwa mfano, tulikuwa na wiki ya kuongelea sauti za vigogo zilivyonaswa. Kulikuwa na mijadala mingi. Kwanza, kama sauti zao nifeki au za kweli. Pili, kwa nini zitolewe hadharani na wasiitane wenyewe na kuambiana kama wanahujumiana. Tatu, hatima yake ni nini baada ya zile sauti kwenda hadharani?

Kabla ya hayo majibu, Bosi wangu wa Mkoa akaona ngoja atuhamishe kwanza kutoka katika mada ile isiyo na majibu na kutuleta katika mada nyingine isiyo na majibu lakini ni nyepesi kidogo na inayoweka tabasamu usoni. Juzi akatoa agizo kwamba wananchi wa kando ya jiji la Dar es Salaam, au wale wanaotoka mikoani wasije mjini mpaka waoge. Ni pale Dar itakapokuwa na wageni kutoka nchi za SADC.

Mjadala ukahama. Makonda bwana! Sasa tunajadili kuhusu kuoga na kupaka mafuta ili turuhusiwe kwenda mjini. Tumeondoka katika kusikiliza sauti tumeenda kuoga. Wakati mwingine najikuta namkubali tu Bosi wa Mkoa. Hana hofu ya kuongea vitu ambavyo vinautata na ambavyo vitabadilisha mada katika jamii.

Kwa jinsi ambavyo Watanzania tuna wepesi wa kusikiliza kauli kama zake nadhani hatutapata majibu kamili ya sauti. Inabidi tuanze kujadili namna ya kuoga, kupaka sabuni, kupaka mafuta na kuingia mjini. Tumeachana na habari ya sauti.

Pia Soma

Wakati tutakapomaliza kujadili kauli ya Bosi wa Mkoa nadhani habari ya sauti za vigogo itakuwa imetoweka. Itakuwa imepitwa na wakati. Ndivyo tulivyo Watanzania. Mada zetu nzito zinapelekwa kwa kasi. Na wakati mwingine jambo kubwa linafanywa kuwa dogo na jambo dogo linafanywa kuwa kubwa. Unaweza kushangaa suala la kuoga kwenda mjini linakuzwa kuliko suala la sauti.

Columnist: mwananchi.co.tz