Leo naweka masihara pembeni. Jana nilikuwa napitia ukurasa wa Instagram wa Haji Manara. Ni msemaji wa klabu ya Simba. Aliposti picha ya mtoto aliyefungwa minyororo huku akilia. Akaandika ujumbe mzito kuhusu kupinga mauaji ya watoto wadogo kule Njombe.
Kilichofuata ni baadhi ya wachangiaji kutuma ujumbe wa kebehi kwa matokeo ya Simba huko Misri, wengine wakatuma ujumbe wa kuhoji kwa nini Simba imefungwa. Nikawaza. Kama mtu anaona matokeo ya Simba ni tatizo kuliko kinachotokea Njombe basi mtu huyo anaweza kudanganywa na mganga kuhusu kupata utajiri au madaraka na kisha akaua mtoto.
Taifa limekwama. Yaani mtu haoni tatizo sana katika mauaji ya mtoto kuliko matokeo ya Simba. Hiki ndicho chanzo cha mauaji. Kwamba tunaona matokeo ya Simba, utajiri, madaraka vinaweza kuwa muhimu kuliko mauaji ya watoto. Taifa limekwama hapa. Wajinga ni wengi katika taifa hili. Kuna watu wengi tunatembea nao, kuishi nao, lakini akili zao zilikufa zamani.
Mpaka tutakapozifufua akili zao ndipo tunaweza kuzuia mauaji ya Njombe. Kinachotokea ni watu kuaminishwa ujinga na wakafikia hatua ya kufanya mauaji. Kitu kibaya zaidi ni kwamba kuna watu wengine nje ya tatizo hilo hawaoni kama ni tatizo kubwa. Unapata hofu na kuamini kwamba siku moja akitumwa anaweza kufanya kweli. Ni mtu kama huyu ambaye katika ujumbe wa mauaji ya Njombe anakejeli matokeo ya Simba au Yanga.
Matokeo yake tukizuia tatizo la Njombe litazuka lingine kwetu Tunduru. Tukizuia Tunduru litaibuka Manyoni. Tukizuia Manyoni litaibuka Tukuyu. Kisa? Ujinga wa watu. Serikali inazuiaje ujinga huu? Wakati mwingine ni vigumu. Tusikomeshe mauaji tu bali tukomeshe wazo la mauaji pia.
Tusipokomesha wazo la mauaji kila siku kitaibuka kitu kipya. Kuna Mganga atasema nywele za wanasheria zinaleta utajiri. Wanasheria wataanza kuuawa. Baadaye itasemwa kuwa vidole vya madaktari vinaleta madaraka, madaktari nao wataanza kuuliwa.
Tatizo tuliua akili zetu. Hazitaki kufikiri tena. Tuna mawazo mfu. Kinachoshangaza zaidi nyuma ya pazia ukienda kusikiliza watu wa Njombe kwa makini unaweza kuambiwa miongoni mwa wahusika wapo wasomi, wanasiasa, matajiri na watu wengine ambao hauwezi kuamini.
Edward Lowassa aliwahi kusema ‘Elimu, elimu, elimu, elimu’. Hakuwa mjinga.