Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Tulihisi January asingefika Januari

67873 Edo+Kumwembe

Tue, 23 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Siasa tamu nyakati hizi. Asikwambie mtu. Tumefika mwaka mmoja na wiki kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu. Rafiki yangu January kapigwa chini katika wizara yake ya ‘mifuko ya plastiki’. Ilitegemewa iwe hivyo. Ilitabirika.

Ilianzia kwake mwenyewe. Wanadai licha ya kuwa mmoja kati ya mabosi wa Kabineti lakini bado ndoto yake ya kuwa Namba Moja iliendelea kuwa pale pale, tena kwa kasi. Namba Moja mwenyewe alikuwa anang’ata meno kila siku alipokuwa akipewa hizo habari na wambea.

Na sasa Baba January naye kaingizwa katika habari za kurekodiwa katika maongezi yake ya simu. Kufikia hapa Namba Moja akaona Baba na mtoto wote wanamchanganya kichwa tu. Hakuwa na jinsi. Akatimiza maandiko. Asingeweza kufika na January, Januari.

Yaani aingie katika mwaka wa uchaguzi na mtu ambaye anataka kuwa Namba Moja? Yaani aingie mwaka wa uchaguzi na mtu ambaye Baba yake pia ana mashaka na U-namba moja wake? Hapana. Haikubaliki.

Lakini pia inabidi tumpongeze rafiki yangu. Amefikaje mpaka juzi? Tulidhani angeondoka zamani. Inasemekana aliingizwa katika Kabineti kwa sababu ilikuwa lazima watu fulani katika chama waingie katika Kabineti.

Wakaingizwa watatu ambao hatukutarajia kuwaona. Wenzake wawili walishatoswa muda mrefu. Alibakia yeye tu katika ‘Plate Number’ za VX. Ilikuwa suala la muda tu. Na yeye mwenyewe alikuwa akiishi katika Kabineti huku akifuata maandiko ya Zaburi 23. ‘Bwana ndiye mchungaji wangu sitapungukiwa na kitu’.

Pia Soma

Na sasa ni wazi kwamba rafiki yangu atahamishia siasa zake Twitter. Ndivyo ilivyo. Siku hizi hakuna mikutano ya siasa lakini kuna Twitter. Tutamsubiri kule. Mimi ni kiongozi wa walioishia darasa la saba. Huwa nachota mambo kule naenda kusimulia maskani kwetu.

Nini kingine kinafuata? Tusubiri. Kwanza nataka nisikie Namba Moja atasema nini wakati akiwaapisha watu wake wapya katika Kabineti. Namba Moja huwa hafichi. Anaweka vitu hadharani. Na kama rafiki yangu hana simile basi atajibu Twitter japo kwa kutumia akili nyingi.

Kitu cha msingi katika nyakati hizi ni kuhakikisha una noti ya kununua gazeti la Mwananchi, lakini pia hakikisha simu yako haiishi bando. Mechi ndio imeanza.

Columnist: mwananchi.co.tz