Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO : Tatizo letu kubwa ni umaskini si upinzani

33345 Edo+kumwembe Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unawasha televisheni yako, unachukua kikombe cha chai, unasubiri uwekaji jiwe la msingi kwa ajili ya barabara nyingi Kimara. Huyu anatoa hotuba, yule anatoa hotuba, mwingine anatoa hotuba. Mpaka inafika zamu ya namba moja naye anatoa hotuba.

Ndani yake kuna vijembe vingi kwa watu wanaoitwa wapinzani. Kila aliyeongea anaweka dhamira ya kukejeli, kukashifu, kuponda watu wanaoitwa wapinzani. Unaishia kutabasamu. Adui yetu ni umaskini au wapinzani?

Unaposubiri hotuba za mapokezi ya ndege inakuwa hivyo hivyo. Bado unajiuliza swali lile lile, adui yetu ni umaskini au wapinzani? Hata kama wanaongea sana, bado adui yetu ni umaskini. Na siku tukiwa matajiri hakuna atakayeacha kupinga na kukosoa mwenendo wa nchi.

Marekani kuna wapinzani, mitume nao walipingwa. Bahati nzuri kwa watawala wetu ni kwamba wapinzani wetu wanaishia kuongea, hawana dola, hawakusanyi kodi. Wanabakia kuwa mbu wanaozunguka sikio ambao wanakukumbusha tu kwamba milango ipo wazi.

Katika hotuba muhimu, bosi wa mkoa anamkumbusha namba moja kwamba mwaka 2020 atamkabidhi wabunge na madiwani wote kutoka chama chake. Hii itaondoa umaskini? Kwa mfano, hili hata likifanyika nchi nzima, itasaidia kuondoa umaskini?

Kuna mambo ambayo namba moja anayafanya. Muhimu kweli. Huwa nafikiria yanalenga katika kutuondoa hapa tulipo kama Taifa. Ukisikiliza hotuba ya tukio zima unahisi kwamba lengo halikuwa kukabiliana na tatizo fulani bali kuwaonyesha watu kwamba wapinzani hawafai.

Hotuba zetu zinajaa majina ya vyama. Hauwezi kusikiliza hotuba ukakosa kusikia CCM, CHADEMA, CUF, UDP. Hakuna hotuba ambayo tunajadili maendeleo tu. Lazima yataingia majina ya vyama. Dhamira yetu ya kushindana kisiasa ni kubwa kuliko kushindana na umaskini.

Hii inanitia hofu. Tunaweza kusimama na kujadili maendeleo tu bila ya siasa? Kinachonisikitisha ni kwamba tatizo la upinzani ndani na nje ya vyama vyetu haliwezi kumalizika. Wanadamu wameumbwa kupinga au kutokubaliana. Ukitembea na hisia za kukataa hali hii muda wote unajipunguzia siku zako za kuishi.

Tukifanya maendeleo tukumbuke kuna Watanzania milioni 55. Waliopiga kura ni milioni 10, wasiopiga kura ni milioni 45 na wanalipa kodi. Habari ya kuzungumzia siasa katika kila mkutano unaohusu maendeleo inachosha. Tatizo letu kubwa ni umaskini sio upinzani.

Ningekuwa namba moja, mikutano ya uzinduzi wa barabara au mapokezi ya ndege nisingewaita CCM, CHADEMA, TLP, CUF wala chama chochote cha siasa badala yake ningewaita watendaji wa wizara na viongozi wa serikali tu.



Columnist: mwananchi.co.tz