Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Swali tunaloulizana kimya kimya kuhusu Dodoma

65402 Edo+kumwembe

Thu, 4 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kaka akanipigia simu kutoka kwetu Tunduru kuniuliza swali fulani ambalo Watanzania tunaulizana kimya kimya. Huyo kaka yangu anapenda mambo ya siasa na kufuatilia kila kinachoendelea huku mjini.

“Hivi akitokea rais mwingine akasema hakuna haja ya kuhamia Dodoma kwa sasa itakuaje?” Akauliza kwa sauti ya kikorofi. Sikuwa na jibu, na hata wewe unayesoma hapa najua huna jibu. Majuzi tulikaa kijiweni tukicheza bao na tukaulizana hili hili.

Wiki mbili zilizopita rafiki yangu mwingine nilisikia akimuuliza mtu swali hili hili. Ni swali maarufu kweli lakini Watanzania wanaulizana kimya kimya. Hakuna dhambi kuuliza hili swali kwani kuna kila sababu ya kuliuliza swali hili.

Kwa mfano, watawala waliopita, watawala wa sasa, wapinzani na wananchi wa kawaida wote wamefundishwa kwamba Dodoma ni makao makuu ya Serikali. Hata hivyo, katika utekelezaji wa kuhamia Dodoma ni Namba Moja huyu ndiye aliyeanzisha safari akatuambia ‘twenzetu’.

Tatizo ni kwamba nguvu ya Namba Moja yeyote nchi hii ni kubwa. Vipi akija mwingine mwenye nguvu kama ya huyu akasema hana mpango wa kwenda Dodoma? Tutabaki tunatazamana. Vipi gharama ambazo tayari tumeingia?

Nadhani kitu cha msingi kwa sasa ni kujaribu kutengeneza sera za Taifa ambazo mtu yeyote atakayeingia madarakani ataambiwa azitekeleze ndani ya muda fulani. Hii inaweza kuondoa hofu ya hili swali ambalo tunaulizana kimya kimya kama vile tunafanya biashara ya bangi.

Pia Soma

Namba Moja wa sasa ametufundisha kwamba tutapata marais wenye tabia tofauti na wasiotabirika. Watapatikana watu ambao watapindua baadhi ya mawazo ambayo tumeyakariri kwa miaka nenda rudi. Ni kama alivyopindua wazo la wenzake waliopita ambao walikuwa wanahofia kwenda Dodoma yeye akasema ‘twenzetu’.

Nchi zetu zinaendeshwa zaidi kwa maamuzi ya waliopo madarakani bila ya kujali waliopita walikuwa wanafikiria nini au wanaokuja watafikiria nini. Ndipo hapo hapo unapokosa jibu la Kaka yangu kutoka Tunduru ‘Akitokea Namba Moja mwingine anarudisha ofisi za Serikali Dar es Salaam tutafanya nini?’ Usidhani lilikuwa swali la kijinga sana. Nilikosa majibu.

Columnist: mwananchi.co.tz