Babu yangu, namaanisha baba yake baba. Aliitwa Mzee Kumwembe. Ndio maana na sisi bado tunadandia hili jina. Alikuwa mzee mmoja jeuri sana. Tulisimuliwa kuwa alikuwa jeuri, kiburi na mkorofi.
Miongoni mwa viwango vya juu vya jeuri kwa mwanadamu wa kawaida ni kuwa jeuri hadi kwa wakwe zake. Mzee Kumwembe alikuwa jeuri hadi ukweni. Angeweza kwenda ukweni na kuanzisha vurugu kubwa. Wakwe zake walikuwa wanamuogopa.
Alikuwa akifika ukweni wakwe zake wanakaa kimya au wanakwenda kwa majirani. Huyu ndiye Mzee Kumwembe halisi. Anaongea kwa sauti ya juu, anatoa vitisho vya hapa na pale kisha anaondoka zake kwa mikogo isiyothimilika.
Baba zangu pia walikuwa wanapata wakati mgumu kwa baba yao. Mzee Kumwembe alikuwa mwindaji mzuri. Alikuwa na shabaha lakini ndani ya uwindaji huo baba zangu walikuwa wanapata wakati mgumu uliopitiliza.
Nilisimuliwa na baba yangu jinsi ambavyo mabega yao yalikuwa yanatumika kama sehemu ya Mzee Kumwembe kulaza bunduki yake ipate balansi kwa ajili ya kuua mnyama aliyekuwa mbele yake. Anakusimamisha mbele, analaza bunduki yake katika bega lako kisha anakwambia uzibe masikio. Anamfyatulia mnyama. Hamkosi.
Miaka ya 1950 Mzee Kumwembe kwa huzuni kubwa akafariki. Kule kwetu Kusini enzi hizo kaburi huwa linaandaliwa na watani. Kaburi la Mzee Kumwembe likaandaliwa na watani zetu kabila la Wamwera. Ilikuwa ni fursa nzuri kwao kumsindikiza Mzee huyu jeuri ambaye alikuwa anawasumbua.
Pia Soma
- Polisi kuuliza kabila la mtuhumiwa kwaibua mjadala
- Polisi Tanzania kuzungumzia sakata la mwandishi wa habari aliyechukuliwa kwa nguvu
- Mwanaharakati China ahukumiwa miaka 12 jela
Katika Tanzania ya leo, kila nikichungulia kwa mbali naona kuna watu wamejaa viburi sana. Ni wakorofi waliopitiliza. Wanajiamini kiasi wanaweza kwenda kufanya vurugu hata ukweni.
Naanza kuwaza kwamba baadhi yetu wakitangulia huenda tukalazimika kuchimba kaburi la Mzee Kumwembe. Kaburi la babu yangu Mzaa Baba. Kaburi la futi 10.