Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Simu ya rafiki yangu mlevi kuhusu bajeti

63099 Edo+kumwembe

Tue, 18 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nikapokea simu ya rafiki mmoja Jumamosi asubuhi. Ana tabia ya ulevi. Sauti yake ilionekana ya kilevi tu. Ana akili nyingi lakini huwa zinayumbishwa na kinywaji. Sikujua anataka kuongea nini hasa. Nikaamua kumrekodi.

“Edo uko poa? Umeielewaje bajeti mwaka huu”? Akaanza na sauti yake ya kilevi. Nikamshangaa sana. Mimi siyo mchumi wala sijui mambo ya uchumi. Pale katika bajeti ile bajeti niliambulia habari ya wigi tu. mengine sijayaelewa. Nikaamua kumsikiliza tu.

“Sikia acha upuuzi. Tangu wakati wa Kighoma Malima kila bajeti tunaambiwa ni bajeti ya wanyonge. Mbona kila siku neno wanyonge linaendelea kuwepo katika vichwa vya habari kama kila mwaka mnyonge anakombolewa?” Akaropoka kwa sauti nzito.

“Hili neno wanyonge lisingekuwepo kama bajeti ya mwaka 1995 iliyoitwa ya wanyonge ingefanya kazi, ikaja bajeti ya mwaka 1996, ikaja ya 97, ikaja ya 98, mpaka mwaka huu inaitwa bajeti ya wanyonge. Kila mwaka, kila bajeti ni ya wanyonge. Au wanazaliwa wanyonge wapya?” Akapumua kwa nguvu. Sikuwa na la kumjibu

“Kila mwaka zinafutwa kodi, halafu zinaongezwa kodi. Mbona kule chini hatutoki? Kule ambako kila mwaka wanasema ni miongoni mwa nchi masikini sana duniani. Mbona hatutoki kule? Kama tunapunguza wanyonge mbona hatutoki kule?”akaendelea kubwata.

“Nakutabiria kuwa bajeti ya mwakani itakuwa ya wanyonge, ya mwaka keshokutwa itakuwa ya wanyonge, kila mwaka itakuwa hivyo hivyo mpaka naingia kaburini. Tatizo la hii nchi siasa ndio inaongoza badala ya taaluma na weledi. Nakwambia aisee,” akaendelea huku nikimsikia akimuagiza mhudumu amuongezee kinywaji. Sijui alilala baa!.

Pia Soma

“Nchi haitapiga hatua kama hatutakuwa wazalendo kwa nchi yetu huku wote tukiamua kuweka siasa kando na kupiga kazi kweli kweli. Nakwambia ukweli rafiki yangu. Wewe nione mlevi tu lakini nakwambia ukweli. Mnyonge wa mwaka 1995 mpaka leo mnyonge kamrithisha mjukuu wake unyonge.” Akabwata huku akionekana ameshatoa dukuduku lake la moyoni.

Baadaye nikaamua kukata simu alipoamua kubadili mada na kuniuliza swali la kijinga huku nikisikia mlio wa glasi inayovunjika. “Vipi Lionel Messi ameshasaini Yanga? Tunatisha sisi katika usajili mwaka huu.” Kufikia hapo nikajua hatuwezi kuongea zaidi.

Columnist: mwananchi.co.tz