Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Simu ya mlevi kuhusu diwani kutiwa ndani kwa kukunja nne

40275 Uchokozipic UCHOKOZI WA EDO: Simu ya mlevi kuhusu diwani kutiwa ndani kwa kukunja nne

Wed, 6 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ghafla nikapokea simu Jumamosi jioni. Mzungumzaji wa upande wa pili aliongea kwa sauti ya kilevi. Kabla sijamdadisi vyema akajitambulisha mwenyewe kwamba alikuwa amelewa lakini anaomba asikilizwe. Sikujua namba yangu ameipata wapi.

“Wewe ndiye Edo Kumwembe?” akauliza. Nikajibu “Ndiyo”. Kwa mbali nikasikia kama ameangusha glasi. “Nataka nikwambie kitu kuhusu mkuu wa mkoa aliyeamuru diwani atiwe ndani kwa kosa la kukunja nne katika kikao chake”. Akasema huku akihema. “Nasoma gazeti hapa nasikia amemtia ndani diwani kwa kosa la kukunja nne katika kikao chake”. Kabla sijajibu akaendelea kwa sauti yake ya kilevi.

“Kwa taarifa yenu nyie waandishi huyu mtu ni kiboko. Amezoea kutoa amri na watu wanazitii. Amezoea watu wamnyenyekee. Baba yake alikuwa waziri wa mambo ya noti zamani. Kwao alizoea kutuma wafanyakazi na wanamtii, sasa kwa nini diwani asimame kama afande katika gwaride?” mlevi aliendelea kubwabaja.

Kabla sijamuuliza kitu akaendelea. “Unakumbuka kabla hajateuliwa kuwa mkuu wa mkoa alitiwa ndani pale Oysterbay kwa kugombana na polisi barabarani? Sasa kama mtu anagombana na polisi halafu kesi inafutwa kimya kimya na baadaye anateuliwa kuwa mkuu wa mkoa mlitazamia nini?” mlevi akaendelea kuongea kwa sauti kubwa.

Kwa mbali nikasikia anamwita mhudumu huku akitoa matusi. Nikajua yupo baa. Wakati nataka kutamka kitu akanidakia hewani na kuendelea “Sasa sikia, huyu mtu ana kiburi chake bwana. Juzijuzi tu rais wangu kasema wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wasitie watu ndani bila ya kuwapeleka mahakamani, lakini yeye hakujali.” Mlevi akaendelea kubwabwaja.

“Hii sheria ikiendelea tutaona mengi sana. Inawafanya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwa wafalme, pia ni sheria ambayo ukiichunguza sana inakwenda ‘against of the constitution’. ‘Actually’ Afrika ina viongozi miungu watu sana.” Mlevi akaweka msisitizo kwa kiingereza. Ningeshangaa kama asingefanya hivyo, pombe na lugha hiyo ni sawa na mswaki na jino.

Mlevi alionekana kuongea kwa kujiamini nikamuacha tu aendelee. “Hata hivyo, nakumbuka na yeye kuna wakati aliwahi kufanyiwa kitu kibaya Morogoro. Ngoja nikusimulie.” Mlevi akabwata. Kabla hajaendelea nikakata simu. Alikuwa hanipi nafasi ya kuongea na nilijua alikuwa anataka kuelekea wapi kuhusu habari yake ya Morogoro.



Columnist: mwananchi.co.tz