DC (Mkuu wa Wilaya) aliyemtolea bastola muuza madafu kanichekesha sana. Kwanza kabisa alikuwa mpinzani. Akawa bingwa wa kutetea haki za wanyonge. Akawa mtu maarufu. Mambo yakaenda vibaya upande wa pili akaamua kurudi upande mwingine. Akapewa cheo.
Sasa ni bosi pale Nanyumbu. Jana niliposoma ile habari tu nikaamini. Kwanza kwa sababu Polisi wenyewe walithibitisha kwamba mheshimiwa DC alitoa bastola hadharani. Pili nikanyanyua simu kumpigia rafiki yangu mmoja anayeishi huko.
“Edo DC anazingua kweli, na kuna mkubwa mwenzake naye yuko hapo hapo wanazingua. Yaani ni shida. Sijawahi kuona jamaa anajivunia cheo kama jamaa.” Rafiki yangu akaniambia. Nikakata simu nikasema sitaandika chochote.
Ghafla nikakumbuka kitu. Majuzi Namba Moja alikuwa amepita huko huko Kusini. Kote huko alikuwa ana maneno mawili makubwa ‘nawapenda sana’ anaongea mistari fulani halafu anasisitiza ‘nawapenda sana’.
Kiburi cha DC kinatoka wapi kumtolea muuza madafu bastola hata kama ana makosa? Kuna mengi hapa, lakini kwanza tuanze kuwachunguza wote waliotoka upinzani kwenda serikalini na kupewa vyeo.
Labda wanahisi Namba Moja hawezi kubadilisha uamuzi wake kwa sababu atakuwa haeleweki.
Kwamba walikotoka walikuwa watu muhimu sana katika siasa za upinzani na kwamba wamerudishwa upande wa pili na kupewa vyeo kwa hiyo wanaweza kufanya wanachotaka kwa sababu wakivuliwa vyeo watarudi walikotoka?
Pia, nikawaza zaidi jinsi ambavyo Watanzania ni watu wale wale tu. Huyu jamaa angebakia kule kule halafu wapinzani wakachukua nchi, ghafla akawa waziri wa mambo ya ndani, si angemkanyaga muuza madafu na kifaru cha jeshi!
Mi nadhani Namba Moja achukue uamuzi anaojisikia tu. Hatutamlaumu. Kumbe ni muhimu kuwapa watu nafasi ili kujua tabia zao bila ya kujali upinzani, ccm, udini, rangi wala kabila. Kuna chui wengi wapo katika ngozi za kondoo.
Najaribu kufikiria jinsi huyu DC wakati huo alipokuwa mbunge wa upinzani angesema nini kuhusu tukio hilo kama lingefanywa na DC mwingine. Ungemsikia anasema “actually this is unacceptable” mheshimiwa Spika. Inabidi tuchukue hatua. “we have to do something”. Angeongea Kiingereza kiingi kumbe ni walewale tu.