Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: STK na STL zinaweza kushiriki Formula One

60477 Edo+Kumwembe

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nipo Dodoma. Nimekuja msibani kidogo. Nimeendesha gari kuja huku lakini nafikiria kurudi na ndege. Hali siyo shwari sana njiani kama unavyofikiria. Kuna ‘nchi mbili’ tofauti ndani ya nchi moja, hasa linapokuja suala sheria za barabarani.

Hawa jamaa wanaoendesha magari ya STK na STL wana kasi ya ajabu. Ni kama hawako chini ya sheria zetu za usalama barabarani. Ndiyo maana katika miezi ya hivi karibuni ajali za STK na STL zimekuwa nyingi barabarani.

Magari kama mawili ya waheshimiwa yalinikosakosa. Wanatanua wanavyojisikia. Ni kasi ambayo ingeweza kuwafanya washindane na kina Lewis Hamilton katika mbio za Formula One. Wao wanazitumia katika njia za Dar es Salaam hadi Dodoma.

Wakati mwingine wanakuwa madereva peke yao, wakati mwingine na mabosi wao. Mwendo ni ule ule. Spidi inaanzia 140 bila ya kujali vibao vilivyoandikwa 50. Ni mwendo wa kasi, hadi unajiuliza mazingira ni yale yale ya hatari yaliyosababisha wataalamu waweke vibao vya ishara za hatari? Au yanaweza kusababisha ajali mbili tofauti; sisi wenye T008XJK tukaumia tofauti na wao wakaumia tofauti.

Wananichekesha zaidi matrafiki. Huwa wanasimama kama wapo katika gwaride pindi magari haya yanapotanua na kushindana kasi. Wanaamini hawayahusu. Wanasumbuana na sisi zaidi. Kinachoshangaza, ajali ya kina STK ikitokea, wanatumia vipimo hivi hivi vyetu na wanamtambua STK kuwa ana makosa. Walikuwa wapi awali?

Ebu tuwageukie mabosi wanaopiga vishoka katika siti za magari haya. Wana haraka zaidi kuliko wengine? Lakini kama wao wana kasi sana mbona maendeleo yenyewe hayana kasi? Wanawahi wapi? Mbona nchi yenyewe haina haraka sana?

Pia Soma

Hapo hapo tunajiuliza tena, kasi hii inamaanisha kila wakati wanakuwa nyuma ya muda? Kama siyo wao basi madereva wao kwa ujumla daima wapo nyuma ya muda. Ukichunguza sana unaweza kukuta bosi anawahi kunywa supu tu Morogoro katika baa anayoipenda.

Nadhani ajali nyingi za magari ya Serikali zinazoendelea zinatokana na nchi moja kugawanyisha sheria zake za usalama barabarani. Kuna wanaoendesha kama wapo katika Formula One na hawaruhusiwi kushikwa, halafu kuna kina sisi. ‘Anyway’ siyo mbaya, siku moja tutakutana kuzimu.

Columnist: mwananchi.co.tz