Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO:Roho mbaya ya kushangaa mishahara mikubwa ipo

63642 Uckozipic

Fri, 21 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Juzi rafiki yangu alinitafuta akiwa likizo Dar es Salaam. Alikuwa ametokea kazini kwake katika mgodi mmoja ulioko mikoani. Akanidokeza jinsi vijana wa Namba Moja wanavyochapa kazi kwa sasa. Wakaguzi wa mara kwa mara wanakwenda migodini kukagua hili na lile.

Moyoni nikashangilia. Tumeibiwa sana katika eneo hilo. Namba Moja anarekebisha mambo. Baadaye akanitia huzuni kidogo. Wakaguzi huwa wanashangaa mishahara yao. Wanashangaa mishahara ya Watanzania wanaopiga kazi migodini. Wanadai ipo juu sana. Hawana shida na mabosi wa kizungu. Bosi mmoja anachukua dola 30,000 kwa mwezi, mwingine anachukua dola 20,000 kwa mwezi. Haina tatizo na hawaoni tatizo. Wanashangaa wanapoona kijana wa Kitanzania anachukua Sh8 milioni kwa mwezi baada ya makato ya kodi. Wengine wanachukua hadi Sh12 milioni kwa mwezi.

Roho zinawauma na kama migodi ingekuwa chini ya Serikali hapo hapo wangemshauri mheshimiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa mishahara hiyo. Ni vile tu hawana mamlaka wala nguvu ya kufanya hivyo kwa sababu wazungu wanaipanga hii mishahara kutokea kwao.

Kwa nini wakaguzi huwa wanashangaa mishahara mizuri? Mshangao unatoka wapi? Roho mbaya tu. Mshangao hautoki kokote zaidi ya roho mbaya. Hatuna mazoea ya kulipana vizuri. Kampuni ya nje inapomlipa kijana wa Kitanzania fedha nzuri kuna watu inawakera. Wanaposikia mgeni analipwa hizo fedha hawana tatizo sana.

Tumeathirika kisaikolojia kwamba Mtanzania hastahili kulipwa Sh20 milioni kwa mwezi. Haiwezekani. Mioyo ya Watanzania wengine imegoma kushangilia. Ni dalili ya roho mbaya au kutojiamini ambayo wengi tunazaliwa nayo.

Unaposikia wanasiasa wanatuambia kuna nafasi za kazi za wageni ambazo zinastahili kufanywa na Watanzania, usiamini kwamba wanataka kazi hizo zifanywe na Watanzania kwa mshahara uleule wa mgeni. Nafasi hiyo akichukua Mtanzania majadiliano ya mshahara yataanza upya. Kama katika nafasi hiyo mgeni alikuwa analipwa Sh20 milioni, basi watataka Mtanzania alipwe Sh5 milioni.

Pia Soma

Kauli zetu za roho mbaya ni kama vile “atatusumbua sana mtaani”. Mwingine atanong’ona “huyu mshahara wake si unaweza kulipa watu wawili na kazi zikaenda?”. Ni kauli za roho mbaya ambazo Watanzania inabidi tuanze kuzitafakari.

Columnist: mwananchi.co.tz