Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Pambano la Waraka na ‘Clip’ limeisha sare?

70438 Edo+Kumwembe

Thu, 8 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tumeachwa katika mataa. Kule katika soka kuna mechi zinamalizika kwa matokeo ya sare. Kuna mechi haiwezekani kumalizika kwa sare. Lazima mshindi apatikane, hata kwa mikwaju ya penalti. Tulidhani katika siasa lazima mshindi apatikane.

Kwa mfano, tumeona Mzee Mamvi amerudi kundini. Ni ishara kwamba pambano limemalizika kwa ushindi wa upande wa Namba Moja. Tumepiga makofi, tumeondoka uwanjani kurudi majumbani mwetu huku tukitabasamu. Tumeuona mwisho.

Lakini hapa majuzi kulikuwa na mechi kali kidogo ya kusisimua. Pambano la Waraka vs Clip za maongezi. Mbona inaonekana kama vile lile pambano la timu ya waraka dhidi ya timu ya ‘Clip za maongezi’ linaelekea kumalizika kwa

sare?. Bado tupo mbele ya televisheni zetu na rimoti zetu hatuoni kinachoendelea na umeme haujakatika?

Wale wazee wangu walikuja na waraka. Ulikuwa mrefu. Uliandikwa kwa umaridadi mkubwa. Baadaye upande wa pili ukaja na clip za maongezi. Hatujapata majibu halisi kuhusu waraka. Yalikuja majibu makali makali kutoka kwa Katibu, basi.

Hata hivyo bado tunajiuliza. Clip zililetwa kwetu kama majibu ya waraka au mashtaka ya kesi nyingine tofauti?

Pia Soma

Vyovyote ilivyo waraka umepita na clip zimepita. Tunaona kimya kimetanda. Mechi inaendelea au imeisha? Nani mshindi? Ina maana clip zilikuwa ni majibu ya waraka?

Sisi wambea wa siasa holela tusingependa pambano liishe kwa sare. Lazima mshindi apatikane. Majuzi nikampigia rafiki yangu mmoja (Sina uhakika kama na mimi nimerekodiwa) akaniambia anadhani pambano lipo muda wa mapumziko.

Akaniambia mpaka kufikia uchaguzi mkuu wa mwakani tutajua nani alishinda katika mechi ile. Huyu rafiki yangu sikupenda alichoniambia kwa sababu sisi wengine tuna hamu mechi imalizike ndani ya muda mfupi. Kuna mambo mengi yanafanyika ndani ya muda mchache.

Uzinduzi wa uwanja wa kisasa wa ndege. Mkutano wa Sadc, hata hivyo nchi huwa inasisimua zaidi yakija mambo kama yale ya Waraka na Clip za maongezi. Wakati mwingine lazima tukiri kwamba tumerithishwa kupenda habari za siasa kuliko habari za maendeleo.

Columnist: mwananchi.co.tz