Siku za mwisho za utawala wa Namba Moja aliyepita, alikuwa amezindua vitu vingi kila kukicha. Miezi yake mitatu ya mwisho, nilikuwa nacheka tu. Safari zilipungua na Mzee akajikita katika uzinduzi wa miradi yake.
Kwa nini? Hakutaka Namba Moja ajaye ahusishwe na miradi yake. Michache ilichelewa na bado haijazinduliwa mpaka leo ingawa ipo njiani. Uwanja wa Ndege ni mmojawapo, lakini mingine mingi alihakikisha kwamba inazinduliwa kabla hajaondoka.
Hii ni kuweka sawa kwamba ‘mradi huu na huu ni mimi ndiye niliyefanya’. Inashangaza kidogo. Kwa sasa tuna tabia hii. Sasa kuna tabia inaendelea. Kuna watu wana kazi nzito ya kutangaza mambo mazuri anayofanya Namba Moja wa sasa.
Kuna watu wengine wanafanya kazi ngumu ya kuzuia hayo maendeleo yasionekane au yapuuzwe. Unaishia kucheka. Ndio maana mtu mweusi huwa haendelei. Anafanya kitu kwa ajili ya kuonekana amefanya yeye. Ndio maana hatutaki mipango ya muda mrefu.
Maendeleo hayapaswi kupigiwa kelele. Zama nazo hazihitaji kelele sana. Mara nyingi ubora wa zama huamuliwa na nyakati pale zinapopita. Nyakati ndizo ambazo zinaamua nani alikuwa Rais bora na kwa sababu zipi.
Kelele zinazoendelea sasa kwamba Namba Moja anafanya makubwa, au hafanyi chochote cha maana zitaamuliwa vizuri zaidi kuanzia 2025. Tabia hii haipo Tanzania tu, katika nchi nyingi nilizotembelea nimekuwa nikiuliza raia wa huko ni rais wao gani aliyepita ambaye wanamkumbuka zaidi.
Pia Soma
- Aliyenusurika tukio la mauaji, asimulia mshale ulivyomuingia mwilini na kukaa nao usiku kucha
- Upinzani Kilimanjaro wawaka ujio wa makada CCM
- Elimu inayotolewa yasaidia kupunguza fedha bandia mitaani
Kwa wale ambao wanaponda kila kitu nadhani na wao wataumbuliwa na muda. Kama ni waongo wataumbuliwa na nyakati. Kama ni wakweli basi watabebwa na nyakati.
Nadhani tungejikita zaidi katika tabia ya kufanya maendeleo bila ya kulazimisha watu wayaone. Wakati mwingine tunapoteza muda kubishana na nyakati. Mara zote nyakati ndizo zinazoamua. Nyakati zikipita zinakuwa hakimu wa kweli. Kwa sasa tunachofanya ni siasa lakini nyakati zikifika basi siasa zitajiweka kando na kila kitu kitakuwa hadharani.