Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO : Noti za Bashir na hotuba za Waafrika

53613 Pic+bashir

Tue, 23 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kilichobaki kwangu ilikuwa kutumbua macho tu. Nikawaza mengi moyoni. Nazungumzia zile noti za Rais aliyepinduliwa huko Sudan, Omar Al Bashir. Majuzi zilikuwa zinasambaa katika video za mitandaoni. Najua zimetutamanisha wengi. Tuache unafiki.

Vyanzo vinapishana kuhusu ukubwa wa dau ambalo limekutwa katika nyumba yake ya kifahari pale Khartoum. Chanzo kimoja kilidai ni Dola za Marekani 130 milioni. Chanzo kingine kilidai kwamba jumla ya fedha zilizokutwa ni Dola 351 milioni.

Ukiona watu wanabishana kuhusu fedha zilizokutwa basi ujue na wao ni wezi. Usiwaamini binadamu wanaokwenda kupekua sehemu halafu wakute fedha au madini. Hesabu itakayoletwa hadharani inakuwa ya uongo. Lazima na wao wachote. Afrika kila mtu mwizi, tunatofautiana katika kiasi na mbinu.

Baada ya kutamani zile fedha ghafla mawazo yangu yakajiuliza. Alizipataje? Haiwezekani kwamba alikwenda benki na kuchukua kama zake. Ni wazi kwamba zilipatikana kutokana na dili mbalimbali za yeye na washirika wake kupitia miradi mikubwa.

Hapo hapo nikawakumbuka raia maskini wa bara la Afrika na hotuba wanazopewa na viongozi wao. Kiongozi aliyeficha mabilioni ya fedha, iwe benki au nyumbani kwake huwa anatoa hotuba ya uchungu akienda kuwahutubia wananchi. Afrika bwana!

Utasikia tu “Sera yetu ya kuondoa umaskini ipo vile vile na nitahakikisha kwamba tunaweka kipaumbele katika afya na elimu. Hili ni taifa tajiri lakini linakwamishwa na watu wachache wanaotaka kuturudisha nyuma.”

Hapo sura inaonyesha kwamba kiongozi anaongea kwa uchungu na wananchi wanapiga makofi. Hawajui kwamba katika chumba kimoja cha nyumba yake amekusanya fedha ambazo kwa asilimia 50 zingeweza kufukuza baadhi ya matatizo yao.

Afrika itaendelea kuwa hivi kwa miaka mingi ijayo. Viongozi wa Afrika ni miunguwatu. Asilimia 90 ya viongozi wa Afrika kitu wanachosema kweli ni salamu tu. wawe watawala au wapinzani, wote wanataka kuweka fedha za Al Bashir chumbani.

Usibishe sana. Asilimia 99 ya watu waliosoma makala hii wanatamani wangekuwa na fedha za Al Bashir chumbani. Ambaye hataki kuwa nazo basi atakosoa tu kuwa “kwa nini hakuziweka benki?” Sio kwamba asiwe nazo!



Columnist: mwananchi.co.tz