Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO : Nkamia, Dk Bashiru wanajituma au wanatumwa?

48450 Pic+edo

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unaishia kutabasamu tu. Shemeji yangu, Juma Nkamia amechachamaa kwelikweli na maono yake ya kuongeza muhula wa urais wa Tanzania. Sitaki kujiuliza kwa nini amechachamaa katika utawala huu na sio ule uliopita. Kuna kitu anatafuta? Sijui.

Halafu ghafla juzi katibu wake wa chama, msomi, dokta mwenye nguvu, Ali Bashiru akamwambia Nkamia atulie “hakuna kitu kama hicho”. Sisi tulioishia darasa la saba tukajikusanya kijiweni kutafakari. Mbona hatuwaelewi hawa watu.

Tukabaki na maswali. Nkamia anapata wapi nguvu ya kuongea kitu kizito kama hiki cha kupindisha demokrasia? Baada ya Mwalimu kukaa madarakani kwa miaka mingi, marais waliofuata wote waliitii Katiba lilipokuja suala la ukomo wa madaraka ya rais.

Alikuwa Mzee ruksa akaondoka zake, akaja Anko Ben akaondoka zake, akaja JK akaondoka zake. Hakukuwa na hofu wala haikufikirika kabisa mtu kusimama hadharani na kudai rais aongezewe miaka ya kuongoza. Nkamia anapata wapi nguvu ya kuzungumzia jambo hili bila ya hofu? Ametumwa, au amejituma?

Kulikuwa na minong’ono isiyo rasmi kwamba ametumwa kwa ajili ya kupima joto. Inadaiwa nyuma ya pazia ilikuwa inasemwa ‘kama joto ni dogo basi tunaweza kufanya mabadiliko, kama joto ni kubwa basi tunaachana nalo jambo hili’.

Ghafla ametokea dokta na kudai kwamba hilo jambo halipo. Bado tunajiuliza, na dokta naye ametumwa au kajituma? Kama hili jambo lipo, dokta ana ubavu kweli wa kuzuia, kama halipo, alikuwa wapi kulitolea ufafanuzi siku zote hizi? Au baada ya kugundulika kwamba uswahilini watu wameshindwa kuafiki?

Mwishowe tunabakia na ‘labda’ nyingi. Nadhani kwa mara nyingine Namba Moja anaweza kuibuka na kufunga mjadala kabisa. Kama si yeye, nadhani wakubwa wengine wanaweza kutufungia mjadala. Muda mwingi kauli za Nkamia na majibu ya wengine imekaa kama kipimajoto tu.

Uchunguzi wangu wa vijiweni unaniambia kwamba bado hatujawaamini sana Nkamia na Dokta. Hatujui kwamba wanazungumza kwa niaba yao wenyewe au ya watu wengine nyuma ya pazia. Ni vyema wakijitokeza wakubwa zaidi wakafunga mjadala.



Columnist: mwananchi.co.tz