Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Ninja Kangi yuko likizo au kabadili utaratibu wake?

34323 Edo+kumwembe Tanzania Web Photo

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ninja Kangi Lugola. Wengine huwa tunamwita hivyo tangu siku ile akiwa mbunge wa kawaida alipotoa kofia ya kininja bungeni na kuivaa huku akijiita ‘Ninja’. Kwa sasa ni waziri wetu wa Mambo ya Ndani. Kuna mtu alitolewa pale akawekwa yeye.

Nakumbuka alikuja na kasi ya ajabu sana. Kasi ya kimbunga. Kila taarifa ya habari ilipowadia mida ya jioni nilikuwa wa kwanza kuwasha televisheni yangu kusikia amesema nini au amefanya nini. Chochote alichofanya kiliniacha mdomo wazi.

Leo angewaumbua polisi hadharani, kesho angemuumbua mkubwa wa polisi hadharani kwa kuchelewa katika kikao chake, keshokutwa angewaamrisha wakubwa wa magereza kwa mikwara. Kila kitu kilikuwa hadharani mbele ya televisheni.

Yule aliyechelewa kidogo akaambiwa atoke nje ya kikao chake nilimwonea huruma sana. Sijui nini kilitokea baada ya pale. Ilikuwa aibu kwa kuangalia tu cheo chake. Mwisho wa siku kamera zilikuwa zinamfuata Ninja Kangi kila alipokwenda. Wale wakuu wa vyombo vya dola ambao sisi tunawaogopa yeye alikuwa anawapa amri za ajabu hadharani.

Sasa hivi naona Ninja Kangi yupo kimya. Sijui yupo likizo…! Vyovyote ilivyo nadhani mwendo wake wa sasa ni sahihi zaidi. Utawala wa Namba Moja umetuacha hoi kwa watu kujaribu kuiga jinsi alivyo. Kumbe Namba Moja ndivyo alivyo na wala haigizi.

Wengine tunapojaribu kuigiza kwa kisingizio cha kwenda na kasi yake hapo huwa tunakosea sana.

Leo tuna watendaji wetu ambao mikwara ni mingi lakini kauli zao hazitakelezeki na utendaji wao wala hauleti tija kama wanavyojaribu kujionyesha katika televisheni. Halafu kuna mtu kama yule Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. Alisifiwa na Namba Moja kwamba anafanya kazi zake vizuri sana huku wengi wetu tukiwa hatumuoni katika televisheni akifukuza watu kazi au kukaripia ovyo.

Nadhani Ninja Kangi ameamua kupunguza spidi na kwenda taratibu. Na huenda nyakati kama hizi akawa anapiga kazi sana kuliko nyakati zile ambazo nilikuwa nakimbilia kumtazama katika taarifa ya habari akipiga shoo za kibabe kwa wakubwa wa vyombo vya dola vilivyo chini yake ambao tunawaheshimu sana.



Columnist: mwananchi.co.tz