Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Ninja Kangi kanikumbusha Super Nyamwela

67318 Edo+Kumwembe

Thu, 18 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

‘Ninja Kangi’ alikuwa katika ubora wake juzi pale Geita. Alinikumbusha viuno vilivyokuwa vinakatwa na mcheza shoo wa zamani wa Bendi ya Twanga Pepeta, Super Nyamwela. Ilikuwa ni shoo ya bure kwa waliohudhuria pamoja na sisi tuliotazama mitandaoni.

Nyakati zimekwenda wapi? Zile nyakati ambazo waziri alikuwa hawezi kufanya vile mbele ya hadhara achilia mbali mbele ya Namba Moja wake. Yaani Al Noor Kassum afanye vile mbele ya Baba wa Taifa, Mzee Ben afanye vile mbele ya Mzee Ruksa au Mzee Mamvi afanye vile mbele ya Ben akiwa Rais? Haikutokea.

Sisi tulioishia darasa la saba tulikuwa tunaamini viongozi ni malaika. Kwamba hawawezi kufanya mambo fulani mbele ya jamii. Kwamba wanaweza kufanya mambo hayo katika klabu za wazee na viongozi (Leaders club) mida ya usiku, wakiwa peke yao.

Kwamba kuna mambo ambayo dereva au watumishi walio chini yako hawapaswi kukuona unafanya. Viongozi walikuwa wanaondolewa kabisa ubinadamu wao. Kama ni kucheza, basi ni taratibu katika muziki wenye mahadhi ya taratibu huku ukitikisa kichwa kidogo. Tena ni kwa dakika chache.

Ninja Kangi kavunja ukimya. Katuonyesha kwamba tupo katika Tanzania nyingine na tuache kukariri maisha. Ametuonyesha kwamba tumehama kutoka kule na tumekuja huku. Huu ni mwendelezo wa matendo mengi ya viongozi wa kisasa kutuonyesha kwamba tumehama.

Tatizo wengine tumezubaa. Bado tunadhani tunaendelea kuishi katika zama za mawe. Nadhani Watanzania wengi wa kizazi changu na kilichopita hawakujiandaa kisaikolojia kuishi hivi ndio maana baadhi ya maneno na vitendo vya mabosi wetu wa sasa tunaona maajabu.

Pia Soma

Tuendelee kuzoea tunachokiona. Tuendelee kuzoea tunachokisikia. Haya ndio mabadiliko ya nyakati na watu wake. Ukiendelea kuishi katika hisia za zamani utateseka. Utakufa kwa presha. Utamuacha mke wako kipenzi na watoto wako.

Utamuacha yule mchepuko wako mrembo akiwa ‘single’ na tukimaliza mazishi yako marafiki zako watamrithi.

Tanzania ya leo sio ile. Hii ni nyingine kabisa. Tuendelee kunywa mtori tu. Nyama tutazikuta chini. Shukrani kwa shoo kabambe ya Ninja Kangi.

Columnist: mwananchi.co.tz