Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO:Nimeunga mkono juhudi, nimekula korosho kilo tano

42507 Uchokozi+pic UCHOKOZI WA EDO:Nimeunga mkono juhudi, nimekula korosho kilo tano

Tue, 19 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nilikuwa ‘Ntwara’ wikiendi hii. Nimerejea jana tu kutoka kule kwetu Kusini. Nilifuata mengine lakini nikaishia kuunga mkono juhudi za mheshimiwa Namba Moja. Nikatafuna korosho za kutosha tu. Safari hii zimetapakaa maeneo mengi.

Misimu iliyopita usingekuta korosho zimechomwa ‘kiswahili’, lakini msimu huu zimechomwa. Nyingine zipo maghalani. Fungu kubwa la korosho unapata kwa Sh500 tu. Zamani akili zao zilikuwa kuwauzia matajiri wa kihindi kupitia kampuni zao. Safari hii mambo mengi yametibua.

Nilichogundua ni kwamba hawajachoma korosho kwa hiyari. Utaratibu mpya wa ununuzi umewalazimisha. Sasa wanajikuta wana korosho nyingi bila hiyari. Nikajikuta nikiwa katika vijiwe vya wahuni ambao mida ya korosho husahau uhuni wao na kwenda kufanya shughuli halali inayohusu msimu wa zao hilo.

Walikuwa wanazungumza chini chini wengine wakiwa na hofu kwamba labda nimetumwa (maagizo kutoka juu) kuwachunguza. Nimewasikia wakinong’ona kwamba mfumo mpya umewakosesha dili na mkoa haujachangamka kabisa.

Walikuwa wakinong’ona kwamba ule ununuzi wa zamani ulikuwa unazipa hoteli wateja wengi, baa zilikuwa zinajaa wateja wengi, pia kulikuwa na kazi za udereva huku vijana wakilamba vibarua vingi. Mfumo mpya wa msimu huu umewaacha chali. Hoi!

Aliyeniacha hoi ni yule aliyenong’ona kwamba ili mambo yaende sawa katika korosho lazima mchezo uchezwe kama soka sio gofu. Nikahoji kivipi? Wakanicheka tu. Mmoja wao akanitafsiria kwamba soka ni mchezo wa wengi, gofu ni mchezo wa peke yako. Unapiga kile kipira bila ya kugusana na mtu. Kwamba lazima wanunuzi wawe wengi asiwe mmoja. Nikacheka sana.

Wakati wakiendelea kuzungumza hayo nilikuwa naendelea tu kutafuna korosho. Mmoja akadai kwamba kuna korosho kibao maghalani lakini zamani zingekuwa zimeisha. Mwingine akadai mjomba wake hajalipwa mpaka sasa. Maneno yalikuwa mengi lakini shauri zao. Nilichojali ni kwamba mkononi nilikuwa naendelea kuunga mkono juhudi za Namba Moja. Alituambia tukiweza tuzitafune.

Licha ya yote hayo uzuri wa Wamakonde bwana ni kwamba wana shukurani. Wakamshukuru Namba Moja kwa zile bei zake za ule msimu mwingine uliopita. Kumbe walikula sana starehe. Msimu huu wanadai mpira umegonga mwamba. Haujaingia nyavuni.



Columnist: mwananchi.co.tz