Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Nilipolazimika kudanganya ili kuepusha aibu

51438 Edo+kumwembe

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Juzi nilikuwa katika treni kutoka Johannesburg kwenda Pretoria. Afrika Kusini hiyo. Kando yangu alikaa mshkaji wangu raia wa Afrika Kusini. Katika simu yangu nilikuwa natazama video iliyokuwa inamuonyesha mheshimiwa mmoja pale mjengoni akitaka uchaguzi wa rais usifanyike mwakani.

Kwamba tuchague madiwani na wabunge tu. Rafiki yangu alikuwa haelewi kilichokuwa kinasemwa na mheshimiwa kwa sababu haelewi lugha ya Kiswahili. Akashangaa kwa nini natabasamu. Nikamjibu “mheshimiwa anaongea pointi sana”. Akaniuliza “Pointi gani?” Nikafikiria kwa haraka namna ya kutunga uongo wa kuepusha aibu kwa Taifa. Nikamjibu kwamba mheshimiwa alikuwa anasema ni bora tupunguze baadhi ya posho za wabunge na kwenda kujenga madarasa na vituo vya afya.

Rafiki yangu ‘msauzi’ akatikisa kichwa kukubali hoja ya mheshimiwa pale mjengoni. Aliumeza uongo wangu. Mlitaka nimwambie ukweli kuhusu kilichosemwa na mheshimiwa? Wakati mwingine tunalazimika kudanganya kwa ajili ya kuokoa aibu ya taifa.

Kwamba yule rafiki yangu ajue kuwa pamoja na suti yake maridadi mheshimiwa aliyechaguliwa kwa kura za wananchi anashauri wenzake wavunje Katiba ambayo aliapa kuilinda na kuitumikia? Uchaguzi wa rais upo kwa mujibu wa Katiba.

Kama ningemwambia ukweli rafiki yangu lazima angeniuliza ni kwa namna gani mbunge aliyetoa hoja alipita katika kura za maoni halafu akachaguliwa kuwa mbunge. Ningejibu nini? Unadhani angetuona Watanzania ni watu wa namna gani?

Rafiki yangu angeniuliza maswali mengi. Angeniuliza kuwa mbona kuna nchi zinafanya vizuri kiuchumi na zinautajiri lakini zinafanya uchaguzi wa rais? Ningejibu nini? Nisingekuwa na majibu. Nikaona nidanganye tu kwa ajili ya kuepusha aibu kwa Taifa.

Unadhani ningemwambia ukweli ningemuachia taswira gani yule rafiki yangu? Watanzania tunaheshimika sana katika nchi za watu, hasa Afrika Kusini ambako tuliwasaidia sana kuwakomboa katika vita vya ubaguzi wa rangi. Leo unadhani wanaamini kwamba Watanzania tuna watu kama mheshimiwa aliyetoa hoja?

Kuna wakati unalazimika kuongea uongo kwa ajili ya kutetea Taifa lako. Sio kila kitu unasema kweli. Ni kama nilivyomdanganya rafiki yangu kuhusu video ya mheshimiwa wa mjengoni aliyetaka kusiwe na uchaguzi wa rais mwakani.

Ningesema kweli kuhusu alichosema Watanzania wote tungedharauliwa. Nadhani nastahili pongezi. Niko juu kama Pierre.



Columnist: mwananchi.co.tz