Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO : Ni kweli, hii kauli ya maagizo kutoka juu inasumbua mitaani

35328 Edo+Kumwembe Eddo Kumwembe

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Rais wangu huwa namwita Namba Moja. Hakuna ubishi katika hili. Yeye ndiye kila kitu katika nchi. Sasa ameanza kung’amua watu ambao wanamuangusha. Majuzi aliongea kitu ambacho kilinikosha. Kwamba siku hizi kila siku watendaji huwa wanasingizia ‘maagizo kutoka juu’.

Kuna watu wanahofia kuchukua uamuzi sahihi kwa sababu kuna uamuzi wa ovyo unafanyika kwa kisingizio cha ‘maagizo kutoka juu’. Kuna watu wanajitengenezea mazingira ya rushwa kwa kisingizo cha ‘maagizo kutoka juu’.

Kuna wafanyabiashara nasikia wanatiwa mbaroni bila ya makosa kwa kile kinachoitwa ‘maagizo kutoka juu’. Kuna watu wengi wanaonewa kwa kisingizio cha maagizo kutoka juu. Nadhani Namba Moja ameng’amua sasa.

Maagizo kutoka juu inamaanisha ni agizo kutoka kwa Namba Moja. Hii ni tafsiri ya zama hizi za utawala wake. Alipoingia madarakani amebadili mfumo wetu wa maisha ya kukariri na sasa huwa tunaamini kwamba agizo likiwa kali basi huwa linatoka kwake. Wakati mwingine inaweza kuwa kutoka kwa Makamu wa Rais au Waziri Mkuu.

Kwa sasa ambacho Namba Moja anapaswa kufanya ni kutupa nguvu watu wa chini kujaribu kuwahoji wanaotujia na kauli ya maagizo kutoka juu. Naamini tukipewa nguvu ya kuhoji hawa watu wanaomharibia Namba Moja kwa maagizo feki nadhani hapo katikati tutakuta maagizo hayo yanaelea.

Kwa asili Watanzania ni wapole. Hawapendi kujiingiza katika migogoro na mtoa maagizo. Lakini kama wakipewa nguvu ya kuhoji maagizo kutoka juu huenda tukaondoa ombwe la kiutawala. Kuna watu wengi wamejinufaisha kwa kauli hii maarufu ya maagizo kutoka juu. Kuna watendaji wengi wanaitumia kuwatia hofu raia au wafanyabiashara kwa kutumia kauli hii.

Naamini ukiambiwa kauli hii utalazimika kujikung’uta chochote kilichopo mfukoni kwa ajili ya kujiondoa katika makucha ya Namba Moja au wakuu wengine. Ina maana kwamba tatizo lako ni kubwa. Kitu cha msingi kwa sasa ni kujaribu kuhoji bila ya kiburi. Mtu akikwambia maagizo kutoka juu tupewe nguvu ya kumuuliza juu wapi?.

Hatuna haja ya kuhoji mamlaka ya Namba Moja, lakini akitupa nguvu ya kuhoji kauli hii ambayo kuna waongo wanaitoa kwa niaba yake basi nadhani atakuwa ametusaidia. Hadi ndani ya chama chake nasikia kuna watu wanaumizwa na kauli hii ya maagizo kutoka juu.



Columnist: mwananchi.co.tz