Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO:Ngoja nimnong’oneze jambo kidogo Namba Moja

48624 Uchokozipic

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Juzi video ilisambaa ikimuonesha Namba Moja akiwa sebuleni kwake. Alikuwa na furaha kwelikweli. Taifa Stars walikuwa wameichapa Uganda na kutinga fainali za Mataifa ya Afrika 2019, zitakazofanyika Misri kuanzia Juni mwa huu.

Namba Moja alikuwa sahihi. Sio kila wakati tuendekeze ‘stress’ zinazotokana na mambo mazito ya hii nchi. Kuna wakati wa kupumua. Jana akawaita vijana wake Ikulu. Hakumsahau pia Bondia wake, Hassan Mwakinyo ambaye siku moja kabla ya juzi alimdunda bondia wa Argentina pale Nairobi.

Michezo inapunguza msongo wa mawazo. Namba Moja alisahau kidogo habari za Standard Gauge. Akasahau kidogo atapata wapi fedha za barabara zake za hewani anazozitamani. Aliweka kando kila kitu akacheki soka kwa dakika 90 vijana wakamfurahisha.

Nilikuwa nataka nimnong’oneze kidogo Namba Moja. Angeweza kuwa na furaha kila ‘wikiendi’ kama wasaidizi wake wangekuwa wanamsaidia katika michezo. Lawama sio kwa wasaidizi wake tu, hata wasaidizi wa wenzake waliopita.

Viwanja ni vibovu. Sehemu za kuchezea katika viwanja vingi vya Ligi Kuu vinatia kinyaa. Juzi Namba Moja kafurahia soka na kulielewa kwa sababu limechezwa Uwanja wa Taifa. Kama mechi ingechezwa Mkwakwani au Majimaji Songea asingeelewa kitu. Watu wa chama chake wamehodhi viwanja vya soka halafu vimekuwa vibovu mno. Hata uwanja tunaojengewa Dodoma asiupeleke katika chama chake. Bora akae nao Serikalini.

Maeneo ya wazi mengi yamevamiwa. Watoto hawana sehemu ya kucheza. Siku hizi wanacheza Playstation tu majumbani mwao. Maeneo ya wazi yamejengwa nyumba au ofisi za matajiri. Wajanja wanabadilisha matumizi ya hati, watoto wanashindwa kucheza.

Kuna mambo mengi ambayo yanashindwa kusogea katika michezo, lakini namhakikishia Namba Moja akitupa jicho lake kwa umakini huko, Serikali itatengeneza matajiri wengi kupitia michezo. Tutapata wanamichezo matajiri watakaokuwa wanachuma Ulaya na kuja kuijenga Tanzania.

Kwa taarifa tu kwa Namba Moja ni kwamba Januari mwaka huu, klabu ya Genk ilikataa dau la pauni 13 milioni kumuuza nahodha wa timu yake ya taifa, Mbwana Samatta kwenda Cardiff. Hizo fedha ni sawa na Sh40 bilioni. Hapo nadhani hakuna kodi yetu, lakini kwa mshahara Samatta angeweza kupata Sh100 milioni kwa wiki. Zote hizi angerudisha nyumbani. Fikiria tukipata wanamichezo kama 100 hivi katika nchi za watu ambao wanalipwa kama hivi. Wangerudisha kiasi gani nyumbani? Geukia huku katika michezo Namba Moja. Nakuamini.



Columnist: mwananchi.co.tz