Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO:Nabisha kwamba Prof Kabudi kateuliwa ‘kumdhibiti’ Lissu

45039 Uchokozipic UCHOKOZI WA EDO:Nabisha kwamba Prof Kabudi kateuliwa ‘kumdhibiti’ Lissu

Wed, 6 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ubishi wa chini kwa chini unaendelea. Kwamba Namba Moja amelazimika kupangua sebule yake na kumteua Mheshimiwa Palamagamba Kabudi kuwa waziri wetu wa Mambo ya Nje kwa ajili ya kupambana na mheshimiwa mwingine wa upande wa pili, Tundu Lissu.

Nilianza kubishana baada ya uteuzi. Watu walisikika wakidai ‘sasa Lissu kapata kiboko yake’. Kwamba akifukua mashimo basi mheshimiwa Kabudi anapita njia hizo hizo kuyafukia. Sikutaka kuamini hilo kutoka kwa mzito mmoja niliyemuamini.

Bosi mpya wa mambo ya nje alikuwa ‘ticha’ wa Lissu. Anaaminika kuwa na ubongo unaofanya kazi sawa sawa. Misimamo yake katika suala la katiba mpya ilijenga mvuto wa ajabu. Kwa sasa ana misimamo mipya kidogo, lakini bado ni mtu imara ambaye angeweza kukaa katika kiti cha Hard Talk akajaribu kumnyamazisha Lissu, lakini kwamba ateuliwe kwa ajili ya kazi hiyo tu? siamini.

Yaani nchi ina mambo mengi ya kufanya katika kujiunganisha na pande zingine za dunia. Waziri wa Mambo ya Nje ni mtu muhimu. Kweli unaweza kuchagua waziri mzito wa nafasi hiyo kwa ajili ya mtu mmoja tu? kweli? Inawezekana vipi! Ina maana baba Masilingi hakutosha katika ile shoo ya Marekani? Ina maana katika Hard Talk yule muendesha kipindi hakutosha?

Hata hivyo, licha ya kuendelea kuwabishia walioamini hivyo huku nikijifanya mtetezi wa Namba Moja na Serikali yetu, lakini juzi nilipata shaka kidogo. Mheshimiwa Kabudi alitumia muda mwingi wa hotuba yake baada ya kuhapishwa akisema kwamba ‘nchi haiwezi kuchafuliwa’.

Hapo palitia shaka kidogo. Huyu Lissu anadaiwa kuichafua nchi huko kwa wazungu. Ina maana alikuwa anazungumziwa yeye? Walipoteuliwa mawaziri wa mambo ya nje waliopita ajenda kuu ilikuwa ni kusimamia uhusiano wa Tanzania na wenzetu wa nje, suala la uwekezaji katika nchi. Hili la kuchafuliwa haliwi ajenda kubwa. Bosi mpya wa mambo ya nje alipoliweka kama ajenda ya kwanza nikajihisi mnyonge. Wale niliokuwa nawabishia walipata hoja.

Hata hivyo bado siamini. Nadhani atachapa kazi kwa mahitaji mengine makubwa ya nchi kuliko kubishana na Lissu. Nyakati zitatuambia. Kwa sasa niko upande wa Namba Moja mpaka hapo mheshimiwa Kabudi atakapojipambanua kwa kazi zake.



Columnist: mwananchi.co.tz