Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Mzee wa kuliamsha ‘dude’ kaibuka kivingine, ana hoja

38175 EDO+PIC UCHOKOZI WA EDO: Mzee wa kuliamsha ‘dude’ kaibuka kivingine, ana hoja

Thu, 24 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nyakati zinakwenda kasi. Nimemkumbuka Mchungaji Gwajima. Wazazi wake walimuita Josephat. Juzi nilimuona akiwa na suti yake maridadi ukumbi wa JK Nyerere pale katikati ya jiji wakati Namba Moja wetu alipoita wadau wa madini. Popote anapokuwapo Gwajima, ni burudani tosha.

Ilinikumbusha wakati ule wa ubora wake. Alikuwa na bifu na bosi wa mkoa wetu. Kila jumapili alikuwa analiamsha ‘dude’ katika madhabahu yake. Nyakati zinakwenda kasi. Sasa hivi yeye na bosi wetu wa mkoa ni washkaji.

Nadhani Mchungaji Gwajima pia, alipitia ule mstari wa Biblia Luka 6:27-38 uliosema ‘Mpende Adui yako’ kisha akasogea ule mstari wa Mathayo 5:43-45 uliosema ‘mpende jirani yako’ akaamua kumaliza bifu lake na bosi wa mkoa wetu. Na bosi wetu wa mkoa siku hizi hana shida na mtu.

Nilidhani baada ya hapo Mchungaji Gwajima angepoteza umaarufu. Kumbe aliamua tu kukaa kimya. Anajua mengi nje ya kazi yake. Siku hizi anaibuka sana katika sherehe za Serikali kama ilivyo kwa viongozi wengine wa dini. Na juzi akaibua hoja nzuri mbele ya Namba Moja. Hoja ambayo itamsaidia Namba Moja kuanzia sasa na kuendelea.

Mchungaji alisema masuala ya madini wasiachiwe wasomi peke yao ambao Namba Moja amekuwa akiwachagua kila kukicha. Kuna watu wamezaliwa na kulelewa katika biashara ya madini. Inabidi wapewe nafasi ya kutoa utaalamu wao katika mambo mengi ikiwamo upatikanaji wa masoko na masuala ya kodi ya madini.

Kwa kuongezea tu, ni kwamba labda wakati umefika kwa Namba Moja kubadili mtazamo wake kuhusu wasomi anaowateua katika nafasi mbalimbali. Takwimu zinatusuta kuhusu idadi ya watu wengi maarufu waliofanya mambo makubwa kwa kutumia akili za kuzaliwa (common sense) kuliko shule.

Na kwa kuongezea tu ni kwamba wenzetu walioendelea walishasahau kuhusu idadi ya vyeti au upara wa kisomi wa mtu anayeomba kazi. Wanaangalia jinsi alivyozikabili changamoto za eneo alilotoka. Ameacha kumbukumbu (legacy) gani?

Hawa akina Nehemia Mchechu nafasi zao zimezibwa na wasomi zaidi, lakini sina uhakika kama nafasi zao zitatendewa haki kama walivyozitendea wenyewe licha ya upungufu wao wa hapa na pale. Mzee wa kuliamsha ‘dude’ ana hoja.



Columnist: mwananchi.co.tz