Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Mzee Membe kabla mate hayajakauka…

66208 Edo+kumwembe

Wed, 10 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Inasikitisha halafu inachekesha. Wiki iliyopita Mzee Membe aliibuka hadharani kukemea utekwaji wa watu unaoendelea nchini. Ghafla juzi tukasikia msaidizi wake naye kaondoka na watu wasiojulikana. Nchi hii bwana!

Mzee wangu alipiga kelele kwelikweli mbele ya vipaza sauti. Akataka wakubwa wenzake wasikae kimya. Kumbe wasiojulikana walikuwa wanamtazama tu. Nadhani walikuwa wanataka kumuonyesha kwamba sio kelele zake, wala za wastaafu wenzake ndizo ambazo zitasaidia wasiojulikana wasifanye kazi zao.

Labda walikuwa hawana mpango huo isipokuwa walitaka kumuonesha tu kwamba tunapita katika nyakati tofauti. Niliandika hapa majuzi kwamba wasiojulikana ni watu waliosomea kazi yao. Wanaijua vyema. Kabla mate yake hayajakauka wakaondoka na mtu wake.

Nadhani labda walikuwa wanamuonyesha kwamba ndio maana wastaafu wenzake wamekaa kimya. Kwamba hakuna wanachoweza kuzuia. Wakati mwingine inachekesha kidogo hata kama tumetumbukia katika dimbwi la hofu. Mwanzoni nilidhani habari hii ni ya kutungwa. Mpaka nilipoona dada wa mtekwaji akizungumza ndipo nilipoamini kwamba ni kweli imetokea.

Baadaye nikawaza, labda mzee mwenyewe alikuwa ‘ameitengeneza’ kuonyesha ukubwa wa tatizo ulivyo? Hapo hapo nikawaza. Kwa nini aitengeneze? Nikaliepuka wazo hilo. Hili tatizo lipo. Juzi tu kuna mtu alikuwa Oysterbay na ghafla akajikuta yuko Mombasa? Tatizo lipo.

Watu ambao wanaonekana kusalimika dhidi ya tatizo hilo mpaka sasa ni viongozi wa dini tu. Maana wao wamekemea lakini hakuna athari kubwa dhidi yao. Inawezekana wasiojulikana wanaheshimu sana dini. Mungu aepushilie mbali.

Pia Soma

Kwa sasa tuone mzee wetu atafanya nini. Niliwahi kuambiwa mahala kwamba na yeye ni mjuzi wa mambo na anayajua kwelikweli. Tusubiri kuona anachoweza kufanya lakini ukweli ni kwamba kuanzia hapa mpaka Oktoba mwakani tutasikia mengi ya kusikitisha, kusisimua na ya kushangaza.

Kadri tunavyokwenda inaonyesha kwamba wasiojulikana wataamua tu kustaafu hii kazi lakini hakuna wa kuwazuia. Inanikumbusha hadithi ya popobawa. Sijui walikwenda wapi lakini ukweli ni kwamba hatukuwahi kusikia kama wameshindwa kazi kwa sababu ya kelele au mbinu za wanadamu kuwazuia.

Tuendelee kunywa mtori, nyama tutazikuta chini.

Columnist: mwananchi.co.tz