Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Muswada wa vyama vya siasa kuongeza umaarufu wa Diamond

39276 Uchokizipic UCHOKOZI WA EDO: Muswada wa vyama vya siasa kuongeza umaarufu wa Diamond

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Watanzania wana tabia ya kutojali sana mambo muhimu na ya msingi. Ni moja kati ya sifa yao kubwa. Wachunguze. Mtanzania hajali kupanda kwa bei ya unga ambao ni chakula chake cha msingi zaidi na wala hajali sana kupanda bei ya umeme.

Ndani ya daladala huyu atashangaa kwamba unga umepanda bei. Mwingine ataguna tu. Mwingine atakuwa katika simu yake akiangalia jinsi mpenzi wa zamani wa mwanamuziki, Diamond Platinumz anavyolalamika kuhusu malezi wa watoto.

Wale Warusi ukipandisha bei ya kinywaji cha Vodka wanaingia mtaani kuandamana. Kenya bei ya mkate ikipanda ni tatizo kubwa na wananchi wanaweza kwenda mtaani. Tanzania umeme ukipanda bei, watu wanaongelea matokeo ya Simba na Yanga au jinsi harusi ya Ali Kiba ilivyopendeza. Ndivyo tulivyo.

Katika siasa kuna Watanzania wengi wameamua kupuuza mambo yanayoendelea, lakini wapo wengine waliokuwa wakifuatilia kishabiki zaidi kama vile wanaangalia sinema. Wengine walikuwa wanajifurahisha na jinsi mambo yanavyokwenda. Haishangazi kuona katika taifa lenye watu 55 milioni wanaojitokeza kupiga kura ni watu milioni tano. Huwa inatokea.

Nilipitia baadhi ya vipengele vilivyomo katika kitu kinachoitwa muswada mpya wa vyama vya siasa. Nikacheka sana. Juzi wameupitisha huku nikiamini kwamba kuanzia sasa itakuwa kama ngumi za mabondia wawili ambazo mmoja atakuwa amefungwa kamba na mwingine ataambiwa amrushie ngumi. Mechi ya upande mmoja.

Kufikia hapo hata wale watu wachache ambao walikuwa wanafuatilia siasa kwa karibu nadhani wataongeza mapenzi yao katika mambo mengine hasa muziki na mpira. Nani ajishughulishe sana katika pambano la siasa ambalo limepangwa?.

Watu wachache waliokuwa wanajihusisha na siasa wataelekeza mapenzi yao zaidi kwa muziki wa Diamond na wale vijana wake ‘wahuni’. Watu watakuwa ‘bize’ zaidi na muziki wa akina Ali Kiba na matokeo ya Simba na Yanga.

Mechi yetu ya upande mmoja katika siasa itamaliza utamu kabisa. Wakati mechi ilipoonekana kama inaelea bado watu wengi hawakupenda siasa, sembuse nyakati hizi ambazo msajili atakuwa ana uwezo wa kuamua Juma maarufu asiwe mgombea halafu John bwege awe mgombea? Nani atapenda kwenda ulingoni kutazama mechi hii ambayo bondia maarufu jina lake limeondolewa halafu amewekwa bondia dhaifu?



Columnist: mwananchi.co.tz