Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO : Mungu ampumzishe vyema Reginald Abraham Mengi

56028 Pic+edo

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Leo hatuchokozani. Tunaomboleza msiba wa baba yetu, Reginald Abraham Mengi. Mwili wake umepokelewa jana jijini Dar es Salaam. Ni huzuni kubwa. Kumpoteza mtu kama Mzee Mengi ni pigo kubwa katika jamii yetu.

Mzee Mengi aliajiri watu wengi, alibadilisha maisha ya watu wengi. Aliwasaidia watu wengi, hasa walemavu. Alikuwa mtu mwema licha ya kuwa na upungufu wake wa hapa na pale. Hakuna mwanadamu aliyekamilika ingawa wapo wachache katika jamii yetu ya leo ambao wanajiona wamekamilika.

Nitamkumbuka Mzee Mengi kwa sababu moja kubwa. Alikuwa mmoja kati ya watu wachache ambao walionyesha nguvu ya ‘chombo cha habari’. Iliwaumiza sana baadhi ya wanasiasa. Mzee Mengi ghafla alikuwa mtu maarufu kuliko wafanyabiashara wenzake, wanasiasa na watu wengine katika jamii.

Kuna wanasiasa au wafanyabiashara ambao waliwahi kufikiria kuanzisha televisheni na redio zao kwa ajili ya kuupiku umaarufu wa Mzee Mengi. Wapo waliokuwa na fedha nyingi kuliko yeye lakini umaarufu wao haukuwa mkubwa kuliko ule wa Mengi kwa sababu yeye alionekana mara nyingi katika ‘screen’ zetu kutokana na mambo mazuri aliyokuwa akiyatekeleza.

Ukiachana na hilo, upande mwingine wa msiba wake ni kwamba kuna watu wanajaribu kudodosa kuhusu kifo chake. Ukisoma kurasa za mbele za magazeti utagundua jinsi Mengi alivyokuwa staa na waswahili wanavyotaka kuugeuza msiba wake wa heshima kuwa kama wa mwanamuziki au msanii fulani hivi.

Unasoma kurasa za mbele za magazeti na kukutana na vichwa vya habari ‘Mengi yaibuka kifo cha Mengi’. ‘Kifo cha Mengi utata mkubwa’. Nadhani inatokana na umaarufu wake na watu wanataka kuuza magazeti. Hili ndilo ambalo limemfanya juzi Mzee JK kuibuka msibani na kuwataka watu waache kusikiliza maneno ya mtaani.

Tumuache Mzee Mengi akapumzike kwa amani. Alikuwa mtu mwema. Kwa sisi ambao aina yetu ya maisha haikuingiliana na aina yake ya maisha, tunabakia kushuhudia kwamba alikuwa mtu mwema. Labda wakubwa wengine wa kiwango chake cha maisha ambao aliwahi kukwaruzana nao.

Vyovyote itakavyokuwa lakini katika mila zetu Waafrika hasa wa Tanzania huwa hatumsemi vibaya marehemu.



Columnist: mwananchi.co.tz