“‘Ninja Kangi’ kumbe bado yupo yupo sana katika anga za kutingisha maafande wetu. Kila siku unapodhania kwamba labda anaweza kunywea kumbe ndio kwanza anawasha moto. Namzungumia Waziri wa Mambo ya Ndani. Tangu siku ile alipovaa kofia ya kininja pale Bungeni wengi wetu huwa tunamuita ‘Ninja Kangi’.
Tangu akalie kile kiti Ninja Kangi yeye huwa upande wa wananchi tu. inatokea mara chache kusimama dhidi ya wananchi akawa upande wa maafande wake. Yeye yupo huku kwetu. Juzi akapiga mkwara mwingine.
Akadai kwamba trafiki wanaosimama barabarani huko mikoani lazima wazipige tochi gari zetu kwa mbele na pia kibao kinachoonyesha kilomita zinazopaswa kuendeshwa katika eneo husika kionekane katika picha.
Ni kweli. Huu ndio uthibitisho halisi wa kujua kama uliongeza kasi katika eneo lisiloruhusiwa kwenda kasi. Picha bila ya kibao cha kilomita sio ushahidi. Vipi kama trafiki alijificha katika pori ambalo gari linaruhusiwa kwenda kasi?
Hapo Kangi anaongea kweli. Sijui kama ana dhamira ya kweli lakini ni wazi kwamba anaowaagiza wanamcheka tu chini chini. Ninja ametoa maagizo mengi ambayo yanatia raha katika masikio ya mnyonge lakini hakuna anayejali.
Vipi lile agizo lake kwamba watuhumiwe wapewe dhamana hata kama ni siku ya Jumamosi au Jumapili. Fanya kosa sasa uone. Ukiingia Ijumaa unatoka Jumatatu kama kawaida. Usiwakumbushe kwamba Ninja Kangi aliwahi kusema unaweza kupewa dhamana Jumapili. Unaweza kupiga kofi jingine.
Pia Soma
- TTCL yaomba Sh1.7 trilioni kuboresha huduma zake
- Nundu: Bila Magufuli TTCL ingekufa
- Bajeti Wizara ya Mifugo na Uvuvi 2019/20 yaongezeka
Maagizo yake ni matamu lakini makamanda wana utaratibu wao ambao ni ngumu kuuharibu. Ni kweli unaweza kubishana na trafiki huku ushahidi wako ukiwa ni kauli ambayo Ninja Kangi aliwahi kuitoa mahala? Sidhani!