Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO : Kwa Nassari nako tunaenda kuzamisha noti nyingine?

47382 Pic+edo

Wed, 20 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Niliacha zamani kusikiliza porojo za watu wanaojiita wazalendo wa nchi hii. Niliacha zamani kwelikweli. Uzalendo ni kuipenda nchi yako, kuzuia ubadhirifu wa mali za Taifa, kuzuia upotevu wa fedha za umma.

Upotevu wa fedha za Taifa ni upi? Ni kama huu uchaguzi wa marudio jimbo la Arumeru Mashariki. Nadhani utafanyika. Tutafanya muda si mrefu, kumbuka tupo mwaka 2019. Mwakani tunafanya uchaguzi mkuu. Kwa hiyo jimbo la yule bwana mdogo, Joshua Nassari litafanya uchaguzi mara mbili ndani ya muda mchache tu.

Uzalendo halisi ni upi? Ni ule wa barua ya Nassari kujibiwa. Kama kweli aliandika katika muda basi angejibiwa katika muda, tusingepoteza fedha. Uzalendo mwingine halisi ni upi? Kama alikuwa hajaandika barua basi mkuu wa mjengo ule wa Dodoma angepiga simu na kusema “Joshua uko wapi? Mbona sikuoni? Unajua siku zikitimia tutaitisha uchaguzi halafu Taifa litapoteza fedha nyingi?”.

Huu ni uzalendo na busara. Joshua angeweza kujibu “Kaka nimebanwa kwelikweli. ‘My wife’ ana katumbo kanasumbua sana. Naandika sasa hivi tuokoe fedha za Taifa”. Huu ni uzalendo wa pande zote mbili. Kama ni kuliwa kichwa kwa lazima Joshua angeliwa mwakani tu, sio mbali.

Huwa natabasamu ninapowaona watu wanaojiita wazalendo wakifukia ardhini kodi za wananchi. Hakuna tunachoweza kufanya kwa sasa. Neno uzalendo ni kama hotuba au picha za Mwalimu Julius Nyerere. Unaweza kulitumia jina hilo pale unapoona lina manufaa kwako.

Inaingia akilini kwenda Arumeru Mashariki kufanya uchaguzi mwaka huu, halafu turudi tena mwakani kufanya uchaguzi? Wenyewe wanasema gharama za demokrasia. Sawa, basi ingekuwa kifo ingeeleweka kwa haraka zaidi. Hili la kunyanyua simu na kukumbushana kwamba tunaweza kupoteza mabilioni ya Taifa kwa sababu ya mtu mmoja anayehangaika na mkewe hospitalini nalo linatushinda kuokoa mabilioni ya fedha?

Hakuna kitu kinachoitwa uchaguzi mdogo hasa kwa mkoa kama Arusha. Fedha zitatumika nje nje. Hadi uone kundi moja linashangilia kwa nguvu ujue tumeshazamisha noti nyingi za walipa kodi ambazo zingesaidia mahala pengine. Zingesaidia ujenzi wa walau madarasa matatu ya wale watoto tunaowaona wanasoma chini ya mibuyu mahala fulani nchini. Uzalendo kazi sana, asikwambie mtu.



Columnist: mwananchi.co.tz