Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO :Kuna sababu nyuma ya umaarufu wa Pierre

49938 Edopic

Tue, 2 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bosi wangu wa mkoa juzi alimshukia vikali mlevi anayeitwa Pierre. Mlevi? Hapana. Tanzania kuna walevi wengi kuliko Pierre. Wengi sana. isipokuwa ndani ya pombe zake, Pierre ni mchekeshaji. Umbo lake na sura yake ni vichekesho tosha.

Labda bosi wangu wa mkoa alikuwa ana hoja. Hata hivyo kabla ya kumwaga hoja zake nzuri angejiuliza Watanzania wa leo walivyo. Wana mengi myoyoni, wana msongo wa mawazo kutokana na sababu nyingi za tofauti. Sababu nyingine zinaanzia hata katika familia zao.

Watanzania wameamua kujiliwaza. Walianza kumtengeneza Dk Shika awaliwaze. Akapata hadi matangazo ya biashara. Wakamtengeneza Mkuu wa mkoa wa Tabora. Asingeweza kupata matangazo ya biashara kwa sababu ya nafasi yake lakini kuna watu walikuwa wanatumia vimbwanga vyake kutengeneza matangazo yao ya biashara.

Sasa wapo na Pierre, wanaamini anawaburudisha. Kampuni zinafanya utafiti na zinajua nani anafaaa kutumika kwa muda husika kufikisha ujumbe wao. Huwezi kuzilaumu kampuni. Zinafanya biashara, na hauwezi kumlaumu Pierre kwa sababu hajajipeleka katika jamii. Jamii ndio imemtaka.

Ukiona Pierre yuko sehemu ujue ameitwa. Ukiona amekwenda kutembelea chombo fulani cha habari ujue ameitwa. Ukiona yupo na watu fulani maarufu ujue ameitwa. Ukiona yupo katika kampuni fulani ujue ameitwa. Hajipeleki.

Labda kitu cha kujiuliza ni kwamba kwa nini Watanzania siku hizi wanapenda sana kujiliwaza kupitia kwa watu wa namna hii? Wamekumbwa na nini? Tukimaliza kutafakari hili tunaweza kupata jawabu la moja kwa moja.

Vinginevyo baada ya Pierre atakuja mtu mwingine katika staili nyingine tofauti. Tutaibuka naye na kumfanya kuwa staa mkubwa. Baada ya hapo atatokea mwingine na kisha mwingine. Tatizo sio yeye, tatizo jamii inataka kutuliza ubongo. Mambo magumu yameanza kuwachosha. Labda hotuba kali za wanasiasa na mikwara mingi imeanza kuwatumbukia nyongo.

Tusisahau pia kuwa kutazama Televisheni za ndani imekuwa ngumu siku hizi. Zimeondolewa katika baadhi ya ving’amuzi. Kumuona Jotti ni ngumu kidogo lakini kumuona Pierre ni rahisi. Unahitaji simu yako tu na Pierre atakupitia katika kurasa za watu mbalimbali maarufu na wasio maarufu.



Columnist: mwananchi.co.tz