Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Kumuona Kenyatta mara kwa mara inafurahisha

66055 Edo+Kumwembe

Tue, 9 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uhuru Kenyatta sijui alikuja kufanya nini pale Chato? Wakubwa wakiitana huwa wanateta mambo mazito. Sisi wadogo hatupaswi kuingilia sana. Imeelezwa alikuja katika ziara ya kawaida sana, lakini yawezekana wakubwa kuna mambo walitaka kuyaweka sawa.

Uhuru kama kawaida yake, akayachukua hayo mambo mazito na kuyafanya mepesi. Akaondoka na tausi wetu. Ndivyo alivyo. Nchi kama Kenya ingeweza kumtia wazimu kama kila jambo zito angekuwa analiweka moyoni.

Ile nchi ina wasomi, ina watu wanaoweza kuongea kejeli sana. Ina watu wabishi. Ina watu ambao kila aliye juu wanamuona ana kichwa kisicho na kitu ndani yake. Yote haya Uhuru anayameza kwa kuweka tabasamu pana na masihara ya hapa na pale pindi anapojitokeza katika uso wa jamii.

Hapa kuna Kijana akipewa wilaya tu anajiona ni zaidi ya Rais wa Kenya. Anabwata, anatukana, anakejeli watu, na kuna yule mwingine alimtolea bastola muuza madafu kule kwetu Kusini. Ndicho kinachomfanya Uhuru kuwa tofauti na baadhi ya viongozi wetu.

Imekuja dhana mpya kwamba uongozi ni mikwara, kutisha watu na kuwakejeli. Sikiliza hotuba za viongozi wetu wa maeneo mbalimbali. Hapa ndipo unapopata hamu ya kumsikiliza Uhuru mara kwa mara kuliko viongozi wengine.

Si kwamba hapati hasira. Hapana. Anashughulika na nchi ambayo ina raia wenye vichwa vigumu kuliko Tanzania. Wakenya wanamkejeli kweli mitandaoni. Hata hivyo ameamua kutokufa na presha. Watu wake wanashughulika na umafia fulani huku na kule lakini yeye ngao yake ni kuishi kama mtu wa kawaida tu katika jamii.

Pia Soma

Ni nadra kumkuta Uhuru akifokafoka hadharani. Nadra sana. Ndio maana watu wanapenda kumsikiliza. Wakati mwingine wanaosikiliza hotuba wanakuwa na matatizo yao, ukiwachanganya na hasira zao unazidi kuwaharibia siku. Wanadamu wanahitaji faraja wanapomsikiliza mtu.

Rafiki yangu mmoja aliwahi kuninong’oneza kwamba ni kwa sababu Uhuru amezaliwa Ikulu. Akaniambia watu ambao wametoka katika umaskini mkubwa wanakuwa na hasira za mara kwa mara zisizo na sababu ya msingi. Akaniambia ni ngumu sana kulelewa katika utajiri, na kisha ukaibuka kuwa tajiri, halafu ukawa na hasira za ajabu ajabu. Inawezekana kweli.

Columnist: mwananchi.co.tz