Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Kumbe Lema anakoposheka mamilioni, hongera zake

51003 Edo+kumwembe

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Afadhali wiki iliyopita imeisha. Afadhali sana. Bosi wa pale mjengoni Dodoma alikuwa amechachamaa kweli kweli. Katika soka tunaweza kusema alilazimisha kupiga hat trick. Yaani alifunga mabao matatu.

Kwanza alianza kwa kutangaza kupiga chini ushkaji wa chombo chake na ustaadhi wa masuala ya hesabu za kikubwa. Professa Assad.

Baada ya hapo akampiga nyundo yule dada mbunge mwenye sauti ya zege kwa kumsapoti ustaadhi. Halafu akampiga nyundo ya kichwa chalii wa Arusha, Godbless Lema asikanyage mjengoni kwake mpaka mwakani.

Soma zaidi: UCHOKOZI WA EDO :Kuna sababu nyuma ya umaarufu wa Pierre

Ndani ya bao la tatu la Lema bosi huyu wa mjengoni Dodoma akataka kufunga bao jingine la kisigino kwa kumkata maini Lema na wafuasi wake. Akasema Lema ana mkopo mkubwa kweli bungeni. Shilingi milioni mia sita na ushee hivi. Bao hili la mwisho kwa mtazamo wangu nadhani limegoma.

Mkopo? Cha ajabu nini hapo? Ni moja kati ya mbinu bora za maendeleo na kujikwamua kiuchumi. Achilia mbali mikopo ya mjengoni lakini mule ndani kuna wabunge tena matajiri ambao pia wamekopa.

Ukija huku nje matajiri kibao wanaishi kwa mikopo. Sisi maskini kila siku tumekuwa tukisisitiziwa kukopa ili tufanye biashara tupate maendeleo na nchi ipate maendeleo.

Soma zaidi: UCHOKOZI WA EDO: Namba Moja alipomsalimia Lema Taifa likashusha pumzi

Sitaki kujadili suala lenyewe binafsi lilifikaje bungeni lakini ukweli ni kwamba kauli ya mkuu wa mjengo imetuacha tukiwa na wivu na mbunge huyu wa Arusha.

Kumbe pamoja na ‘uhuni’ wake wote bado anakopesheka? Na kumbe anaweza kulipa deni analodaiwa?

Wakati fulani wakubwa wetu tangu tawala zilizopita huwa wanajisifu wakisema ‘Nchi yetu inakopesheka kwa wahisani’. Huu wimbo umekuwa ukisikika sana hata katika miaka ya karibuni.

Kama ni kweli tatizo linakuja wapi kama wabunge wa vyama vyetu vya siasa nao wakiwa na mikopo binafsi? Mimi nilidhani hii ni sifa nzuri.

Soma zaidi: UCHOKOZI WA EDO:Ya Assad na korosho, mambo ni mengi muda mchache



Columnist: mwananchi.co.tz