Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Kule katika kamari ya Kaisari tumuachie Kaisari

41724 Edo+Kumwembe UCHOKOZI WA EDO: Kule katika kamari ya Kaisari tumuachie Kaisari

Fri, 15 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Alisema kiongozi mmoja wa dini mbele ya Namba Moja wiki kadhaa zilizopita akipiga vita kamari. Akataka tusimamishe matangazo ya kamari. Baada ya siku tatu tu tukapewa habari kwamba matangazo ya kamari katika redio na televisheni yamesimamishwa.

Ni kweli tumevamiwa na kamari. Kuna kamari za bahatinasibu halafu kuna zile za soka. Wanaotangaza wanalipa kodi kubwa katika Serikali ya Namba Moja, hata wanaocheza pia wanalipa kodi kubwa.

Palepale Namba Moja aliutupa mzigo kwa Waziri Mkuu. Baada ya siku mbili matangazo yakapigwa marufuku ingawa kamari yenyewe inaendelea kuchezwa. Akili ya kawaida inanituma kwamba ingekuwa vyema kama ya “Kaisari angeachiwa Kaisari” mwenyewe kama maandiko ya Biblia yalivyosema.

Kwa sasa Serikali inakosa kodi ya matangazo ya kamari. Imeamua kujichoma sindano yenyewe. Sina uhakika sana kama wachezaji watapungua. Ninachodhani ni kwamba viongozi wa dini wangeendelea na kazi yao nzuri ya kuhamasisha watu wasicheze kamari na waishi katika maadili mema.

Kuna tatizo hapa la baadhi ya viongozi wa dini kuanza kuwa wavivu wa kutimiza wajibu wao, badala yake wakataka Serikali itengeneze njia ya mkato kuwasaidia katika mahubiri huku Serikali yenyewe ikijinyima kodi.

Kwa mfano, vipi viongozi wa dini wangetoa wazo kwa Namba Moja kuwa watu wanakunywa sana pombe hivyo viwanda vifungwe au visiruhusiwe kutangaza biashara? Namba Moja angetekeleza hili? Sidhani. Kampuni za vilevi ni miongoni mwa walipa kodi wazuri katika nchi hii.

Nadhani katika haya mambo kwa kiasi fulani kila mtu atimize wajibu wake. Huyu mmoja ahubiri kwa nguvu kwamba kamari ni mbaya, yule mwingine afumbe macho akusanye kodi. Yule mwingine ahimize kwa wazazi kuwalea watoto wao kimaadili zaidi na wasicheze kamari huku mwingine akikusanya kodi kwa hao wanaocheza.

Haya mambo kwa sasa hayawezi kwenda pamoja. Namba Moja ajue anachokitaka katika Serikali yake na viongozi wa dini wajue wanachokitaka katika mahubiri yao. Tukijaribu kupeleka haya mambo kwa pamoja hasa katika nyakati hizi ambazo Namba Moja anajitahidi kuwavimbia wazungu na kutaka tujitegemee nadhani tunaweza kujitengenezea kitanzi mbele ya safari. Baniani mbaya lakini kiatu chake dawa. Ya Kaisari tumuachie Kaisari.



Columnist: mwananchi.co.tz