Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Krismasi njema wote, hasa kwa Mohamed Kiluwa

33474 Edo+Kumwembe Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Krismasi imeliwa jana duniani kote, lakini kipindi chote hiki ni cha Krismasi. Wengi wamefurahi, lakini inawezekana kuna mwanadamu mmoja amefurahi zaidi duniani. Jumatatu jioni wakati wenzake wakinunua kuku, yeye alikuwa anakaribia kuta za gereza.

Ni yule bwana Mohamed Kiluwa. Mfanyabiashara ambaye alituhumiwa kumuhonga waziri mheshimiwa sana. Inadaiwa alimuhonga Sh90 milioni. Na kama ingekuwa katika mchezo wa soka basi tungesema kuwa kila dakika ya mechi alikuwa amehonga kiasi cha Sh1 milioni.

Ameponaje bwana Kiluwa? Inashangaza kidogo. Utuhumiwe kumuhonga waziri Sh90 milioni, waziri awe mshtaki, fedha afikishiwe halafu bado upone? Unahitaji kuwa na bahati ya mtende. Sijui haki imesimama vipi lakini naiwazia bahati yake.

Sijui sana mambo ya sheria, lakini kitendo cha mtuhumiwa kufikisha hizo fedha kwa waziri, akapelekwa mahakamani, halafu hakimu akamuona hana hatia na inabidi arudishiwe fedha inashangaza sana. Mtuhumiwa anastahili kuwa mwanadamu mwenye bahati na hakimu pia anastahili kupongezwa kwa kuamini alichokiamini.

Niliposoma mwenendo wa kesi nikagundua kuwa mtuhumiwa alikuwa na viwanja vyake viwili Pwani na alikuwa anavimiliki kihalali. Waziri pia amekiri hilo. Kuna sauti ilisikika ikimwambia mheshimiwa apokee tu hizo fedha lakini sio hongo. Kwa nini mheshimiwa alipokea halafu akasema amehongwa?

Kwa vyovyote ilivyo, nadhani katika suala zima kuna uwezekano mheshimiwa alitengeneza mazingira ya kuonekana mwaminifu zaidi. Katika mazingira ya sasa iandikwe hadharani ‘Waziri akataa rushwa ya milioni 90’ nadhani inakuongezea sifa nyingi na uaminifu mkubwa.

Pamoja na yote haya, mheshimiwa waziri ni mmoja kati ya mawaziri wanaofanya kazi yao vema sana, ni mchapakazi mzuri. Amemaliza migogoro mingi ya ardhi. Ni waziri ambaye amekuwa suluhisho la wanyonge. Ni kwa nini au kulikoni yaje madai au tuhuma za kumbambikia kesi nzito mfanyabiashara huyu? Pengine hili ni swali la kujiuliza sana baada ya hukumu ya juzi.

Hata hivyo, hakuna la kuongeza zaidi ya kumtakia Krismasi njema Bwana Mohamed Kiluwa ambaye saa hizi angekuwa anazungumzia gerezani.

Inawezekana kuna watu wengi kama yeye wako nyuma ya kuta za gereza kwa kesi za namna hii. Yeye ana bahati sana. Na ndio maana haikushangaza kwa ndugu zake hasa mkewe kuangua kilio cha furaha baada ya uamuzi wa hakimu. Jumatatu ilikuwa hukumu, Jumanne Krismasi na bado amenusurika katika kesi ya kumhonga waziri Sh90 milioni!



Columnist: mwananchi.co.tz