Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Korosho zina ‘Breaking News’ nyingi kuliko CNN

41472 Uchokozipic UCHOKOZI WA EDO: Korosho zina ‘Breaking News’ nyingi kuliko CNN

Wed, 13 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mashujaa wetu waliokwenda katika vita ya Kagera kule Uganda waliifanya kazi yao vyema, wakarudi na kupokewa kishujaa. Mashujaa wetu walioagwa kwenda kununua korosho bado hawajarudi. Bado hatujawapokea kishujaa. Sijui nini kinaendelea.

Hata hivyo kila siku tunapokea ‘habari zilizotufikia hivi punde’ maarufu kama Breaking News kutoka katika vyanzo tofauti. Kiukweli zinatuchanganya sisi wafuatiliaji wa filamu ile ya kusisimua. Majuzi yule mwanasiasa mwenye mdomo mpana, rafiki yangu, Zitto Kabwe amekuja na habari mpya kabisa, kwamba Taifa limetapeliwa na kampuni fulani hivi.

Akatoa ufafanuzi wake ambao binafsi sijauelewa. Taifa linatapeliwa vipi? Kweli kwa mabilioni yale ya fedha? Ilikuaje kampuni ya nje ikapewa tenda wakati tulishaaminishwa korosho tutanunua wenyewe na tunaweza kuzibangua hata kwa meno? Ghafla imekuaje tumekuja kusikia habari ya kampuni ya nje, mbona tunachanganywa?.

Kabla ya hapo Waziri Mkuu alikuwa na taarifa yake katika kipindi chake cha maswali na majibu. kabla ya hapo mbunge mmoja wa upinzani akiwa bungeni Dodoma alidai kwamba alikuwa tayari kuachia kiti chake kama korosho hazikununuliwa kwa bei ya chini tofauti na ile ambayo aliitaja Namba Moja wakati anawaaga mashujaa wetu.

Kuna Breaking News nyingi kwelikweli kuhusu korosho. Hatujui tumuamini nani. Ukisikiliza stori za watu wa Mtwara na Lindi pindi wakija mjini unakata tamaa. Unasimuliwa madudu mengi kuhusu ununuzi wake, wengine wanakwambia wameingia hasara kubwa kwa utaratibu uliotumika mwishoni mwa mwaka jana.

Wote hao sitaki kuwasikiliza. Natamani tuwapokee mashujaa wetu walioenda kusimamia korosho kama tulivyowaaga. Ni vizuri Taifa likipata mrejesho kuhusu suala la korosho kama tulivyowaaga mashujaa wetu kishujaa wakati wakiwasha magari yao makubwa kwenda kununua korosho.

Vinginevyo tutaendelea kupokea Breaking News nyingi. Kuna ambazo zinatolewa na wanasiasa, nyingine zinatolewa na watu wa kawaida. Kitakachotutoa katika uvumi ni mrejesho tu kutoka kwa Namba Moja. Tukifahamu kwamba tumepiga au tumepigwa basi tunajifuta vumbi na kuendelea na maisha mengine. Wakati mwingine itatutia uimara wa kujiandaa na msimu ujao. Kuna baadhi ya mambo hayatakiwi kufanyiwa mzaha au majaribio.



Columnist: mwananchi.co.tz