Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO:Kila Aprili kuna pesa inapigwa kwa staili hii

60081 UCHOKOZIPIC

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tukiwa katika kijiwe chetu cha bao kinachotukusanya watu wengi tulioishia darasa la saba, juzi tuliwaza jambo. Mimi ndio huwa nakuwa kiongozi wao wa kutafakari. Wananiamini kwelikweli.

Juzi nikaongoza mjadala kuhusu barabara zetu. Ikifika Aprili mvua zinanyesha sana. Barabara zetu zinaharibika. Katika barabara za lami kunakuwa na viraka ambavyo viliwekwa mwaka mmoja uliopita kwa tatizo hilo hilo la mvua. Huwa vinang’oka na mashimo yanarudi vile vile.

Baadae unaanza kuona magari yakifukia tena yale mashimo kwa kiwango cha lami. Moyoni unaamini kwamba tatizo limepata suluhu kwa sababu kiraka cha barabara ya lami kinawekwa kwa lami. Kwa nini kisidumu?

Mvua za Desemba au Aprili zikirudi kiraka kinashindwa kuhimili. Kinaondoka na lile shimo maarufu linarudi. Nadhani wale mabosi wenye wajibu wa kukiziba tena kile kiraka huwa wanatabasamu. Tenda imejileta tena. Wanajua namna ya kuigawa, wanajua bajeti ya dharura inavyokwenda, pesa inapigwa.

Swali la msingi linakuja, kwa nini mashimo maarufu ndani ya barabara za Dar es salaam yameshindwa kudhibitiwa? Kwa nini mashimo kila yakizibwa yanarudi baada ya mvua? Hakuna mashimo mapya katika barabara zetu. Mengi ni yale yale ambayo yalitengenezwa baada ya mvua kubwa zilizopita.

Ni kama mradi fulani hivi ambao unafurahiwa na mabosi wanaohusika katika kuziba. Kila mtu kwa muda wake nadhani anajua mashimo yaliyopo katika barabara za lami mtaani kwake na miaka nenda rudi huwa hayawezi kuondoka moja kwa moja.

Pia Soma

Kwa upande wangu, pale Mwananyamala sokoni, kuna yale yaliyopo mbele ya Baa ya Maeda Sinza, pia yapo yale ya barabara ya kuelekea Sinza Makaburini na kwingineko. Sidhani kama limekosekana suluhisho la kudumu. Nadhani bajeti za dharura zinazopita baada ya mvua huwa zinapokewa kwa mikono miwili na wapigaji maarufu wanaohusika katika kurekebisha.

Ukitafuta jibu la ukweli watakujibu kwa Kiingereza kingi. Watakupa sababu nzito za kiuhandisi lakini ukweli ni kwamba hawajakosa suluhisho la kudumu. Wanafurahia tu kuona mvua inaacha mashimo na wao wanapata mianya ya kupiga pesa. Ndivyo nchi ilivyo. Usione watu wanaendesha magari ya kifahari. Mengine yanatokana na faida za mvua.

Columnist: mwananchi.co.tz