Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Kikapu cha sadaka kilipojaa noti za elfu ‘fasta’

54726 Edo+Kumwembe

Tue, 30 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jana niliandika mambo magumu. Leo tunapoza kichwa kidogo. Maisha hayahitaji presha sana. Tutakufa siku sio zetu. Bado nipo katika ziara ya Namba Moja pale Mbeya. Anatembeza hotuba zake na kufanya mambo ya kijamii kule Nyanda za Juu Kusini.

Hivi mlikiona kikapu cha sadaka alichokuwa anatembeza Namba Moja pale Mbeya? Nilicheka sana. Wanadamu bwana! Juzi Namba Moja akajipa jukumu la kukusanya sadaka katika Kanisa Katoliki pale Mbeya. Nikawa nakichungulia kile kikapu.

Kile kikapu kilikuwa kimejaa noti za Sh10,000 kibao. Watu wa kawaida nao walikuwa wametoa noti za Sh10,000. Kuna yule ambaye alikuwa amejipanga kutoa Sh500, alipoona Namba Moja kashika kikapu mbele yake akachomoa noti ya elfu kumi akaweka. Moyoni akabakia na majuto.

Kuna mwingine ambaye inawezekana alikuwa na Sh10,000 tu akaitoa hiyo hiyo. Akalazimika kutembea kwa mguu kutoka Mwanjelwa, Mama John, Nzovwe, Sai mpaka akafika kwao Uyole. Namba Moja anatisha bwana. Kumtazama katika televisheni ni jambo moja tofauti kabisa na anaposimama mbele yako akiwa na kapu la sadaka.

Namba Moja anatisha asikwambie mtu. Kama kikapu kingetembezwa na mtu mwingine basi raia wangetoa shilingi mia tano walizozoea. Tumefundishwa kwamba sadaka zinakwenda kwa Mungu, ina maana kuna raia wanatishwa na Namba Moja kuliko Mungu? Mbona siku nyingine hawatoi noti nyekundu.

Mara nyingi Namba Moja huwa anajigamba kwamba anafanya kazi za Mungu. Ni kweli anazifanya sana lakini juzi ndio alifanya kazi ya Mungu hasa. Alimkusanyia noti zake vyema kabisa. Wanadamu wanafiki waliumbuka ghafla.

Ujumbe wangu hapa ni kwamba tufanye mambo mengi kwa hiyari yetu na sio kumuogopa mtu. Hapa ndipo tunapokosea. Kwa mfano, Namba Moja huwa anamaliza matatizo ya akinamama wachache wanaojitokeza na kilio kikubwa mbele yake wakielezea shida zao. Anawasaidia. Na wasaidizi wake wa mikoani wanauvaa unafiki wa kusaidia haraka haraka. Kumbe kama bila yeye akinamama hawa wangeishia kuzurura katika milango ya maofisa wetu wa mikoani bila mafanikio. Jibu lao ni lile lile kupitia kwa Sekretari ‘bosi ana kikao kirefu’.



Columnist: mwananchi.co.tz