Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHOKOZI WA EDO: Karia ametia chumvi katika chai, akaweka sukari katika chipsi

39936 Edo+kumwembe UCHOKOZI WA EDO: Karia ametia chumvi katika chai, akaweka sukari katika chipsi

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Rafiki yangu, Wallace Karia. Ndiye bosi wetu wa soka hapa nchini. Juzi alivaa suti nzuri kwelikweli pale Arusha katika mkutano mkuu wa watu wake wa mpira. Akaanza kuongea vizuri kama suti zake. Baadaye akamalizia maneno ambayo hayakuoana na suti hiyo.

Kule kwa wakubwa wa mpira, Fifa huwa hawataki siasa. Mchezaji yeyote akifunga bao akaonyesha maandishi yenye mtazamo wa siasa anafungiwa. Kama ndani alivaa fulana yenye picha ya mwanasiasa au ujumbe wa siasa anafungiwa, akishangilia kwa ishara za kisiasa anafungiwa.

Fifa hawataki kuchanganya mambo. Wameacha soka iwe soka. Juzi pale Arusha, rafiki yangu Karia ‘akaropoka’. Kwa sauti ya juu huku akitaka watu wamskie vyema akasema “Nitahakikisha watu wanaojifanya akina Tundu Lissu wote katika soka nawaondoa”.

Hapo alikuwa anaweka chumvi katika chai. Baadaye akatoa ufafanuzi wa kauli yake akadai alisema hivyo kwa sababu kuna mtu katika mpira (Michael Wambura) anaikashifu sana TFF kama Tundu Lissu anavyoikashifu Serikali. Kufikia hapo akawa ameweka sukari katika chips. Tangu lini bosi wa TFF akageuka kuwa Humphrey Polepole?

Sijui kauli ya Karia hapa itafananishwa na mfano upi kati ya ile inayochukiwa na Fifa, lakini tayari wenye mambo yao wameshaanza kutoka hadharani wengine wakisema wanaitafakari kabla ya kuchukua hatua na wengine wakiilaumu.

Wanailamu kwa kuwa bila shaka imetolewa katika eneo lisilo sahihi na mtu asiye sahihi ambaye hakutarajiwa. Kauli kama hiyo ingetolewa na Polepole na kutupiwa katika mitandao ya kijamii pengine wengi wangeifungua, kuitazama na kuiacha kama ilivyo kwa kuwa wangeihusisha na siasa, lakini sasa imetolewa katika soka! Ndipo mkorogo ulipoingia.

Imewagusa kwa kuwa Rais wetu huyo ni kama amechanganya viungo muhimu katika vyakula visivyoendana, matokeo yake ameharibu ladha sahihi.

Haya ya siasa tungeyaacha katika siasa. Wadau wa soka wakaendeleza soka lao. Yapo mengi ya kujadili kwa mustakbali wa mchezo huo ambao bado hatujaufikisha kunakotakiwa. Muda mwingi utumike kufanikisha maendeleo ya soka. Ya siasa waachiwe wenye siasa zao.



Columnist: mwananchi.co.tz