Jinsi ilivyovutia wakati Namba Moja alipoita wachezaji wa Taifa Stars pale kwake Magogoni. Akawaeleza alivyokoshwa na ushindi wao dhidi ya Uganda ambao ulitupeleka michuano ya Afcon kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39. Ilivutia.
Tukio kubwa. Wachezaji na baadhi ya viongozi wakapewa viwanja kule Dodoma. Tulikuwa tunakodoa macho katika televisheni. Ukifungua chaneli hii unakuta tukio lipo live. Ukifungua kwingine unakuta tukio lipo live. Unajivunia.
Leo timu imekwenda Misri inakaribia kuanza kushiriki lakini hauwezi kuona live. Hauoni chochote. Hakuna mwandishi wa magazeti wala Televisheni. Kalamu zetu na peni haviwezi tena kuvuka mipaka. ‘Media’ zipo hoi kwa sasa. Zipo taabani. Zinajaribu kujikaza lakini hali halisi ndiyo hii.
Ubavu wa media zetu kwa sasa ni kwenda kubanana magogoni, au maeneo ambayo wakubwa wanafikika kirahisi. Hatuwezi tena kwenda nje ya mipaka kwa sababu vyombo vya habari havina uwezo wa kifedha tena.
Waandishi wetu walipaswa kujazana Cairo lakini imeshindikana. Biashara imeshuka kwa sababu nyingi. Uwezo wa watu kununua magazeti umeshuka. Lakini wale waliokuwa wanatangaza magazetini kuanzia taasisi binafsi na Serikali yenyewe wamechomoa matangazo. Kampuni zinapunguza wafanyakazi. Kuna sababu nyingine ya biashara hii kutofanya vizuri lakini naiweka mfukoni.
Matokeo yake ni haya hapa. Tukio kubwa la timu ya Taifa ya mpira wa miguu inayoshiriki Afcon kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980 halina waandishi wa habari. Media zipo hoi. Hakuna mwenye ubavu wa kupeleka waandishi mpaka sasa. Ni huzuni.
Pia Soma
- Maonyesho ya biashara ya sabasaba kuanza Juni 28
- Kesi mauaji ya Dk Mvungi yapata hakimu mwingine
- Wabunge wa CCM walalamikia Serikali kuchukua vyanzo vya halmashauri
Inabidi media zianze kusaidiwa. Kama ambavyo Namba Moja ameanza kuwasadia wafanyabiashara wengine ni wakati wa kuisaidia pia ‘biashara ya habari’ ambayo nayo ni kama biashara nyingine isipokuwa inabeba jukumu kubwa la kuisadia jamii kwa maadili tofauti.